Na Mwandishi wetu- Kilimanjaro
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha changamoto za usimamizi wa mirathi zinazowakabili kina mama wajane zinapata ufumbuzi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akikabidhi nishati mbadala ya kupikia (majiko ya gesi) kwa kina mama wajane katika kijiji Kiriche, Kata ya Makuyuni wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema kuwa, Serikali inatambua changamoto ambazo wajane wanapitia katika usimamizi wa mirathi na kuwataka kutokata tamaa wala kuvunjika moyo.
“Tunafahamu kina mama mnakutana na changamoto nyingi katika eneo la mirathi, msimamizi wa watoto pindi baba anapofariki na wengi wenu mmekuwa mkikosa haki zenu kwa kutokana na kukosa elimu kuhusu mirathi nipende kuwahakikishia kwamba Serikali ipo pamoja na nyinyi,”Alisema Ummy.
Pia Naibu Waziri huyo alisema kuwa, katika kuhakikisha mapambano ya utunzaji mazingira hasa mapambano ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanafanikiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja na kampeni maalum ya nishati mbadala ya kupikia hatua itakayosaidia uhifadhi wa mazingira pamoja kuepikana na madhara yatokanayo na matumizi ya mkaa na kuni.
"Sisi kinamama ndio tunabeba mzigo wa kupika lakini wakinababa wao wanasubiria chakula mezani lakini hawajui tunapitia mchakato gani wa kupika maeneo mengine tunachafua mazingira kwa kukata miti ili kupata kuni hivyo sasa tunakuja na kampeni ya nishati mbadala ya kupikia" Alisema Naibu Waziri Ummy.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum, Gladness Mfinanga aliwataka kinamama hao kutumia majiko hayo kama yalivyokusudiwa ili kulinda mazingira.
“Kutokana na uharibifu wa mazingira kusababisha ukame na joto kali niwasihi wananchi tutunze mazingira kwa kuotesha miti katika maeneo yetu ya makazi,”Alibainisha.
Naye Mkazi wa Kitongoji cha Kifula, Kata ya Makuyuni, Mwanasha Kidaya aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile nishati safi ya kupikia akisema kwao imekuwa faraja kubwa kwani hukumbana na changamoto nyingi.
“Tunashukuru sana na tunaahidi kutokuharibu mazingira awali tulikuwa tunapata changamoto ya kupata kuni au mkaa hasa wakati wa msimu wa mvua lakini sasa upatikanaji wa nishati hiyo ambayo ni rafiki wa mazingira utakuwa msaada kwao,”Alipongeza mkazi huyo.
Aidha Mkazi wa Kitongoji cha Saidingi, Kata ya Makuyuni, Zuena Sado aliwahimiza wananchi kuhamasika kutumia nishati hiyo mabadala na rafiki wa mazingira akisema huo utakuwa mwarobaini kwa baadhi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kuweka afaya zao katika hali ya usalama.
0 Comments:
Post a Comment