Mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli Mrakibu wa Polisi (ASP) Rashid Nchimbi amesema kwamba msingi wowote wa maendeleo unatokana na hali thabiti ya usalama.
Hayo aliyasema mapema leo Desemba 02,2023 ofisini kwake wakati anaongea na baadhi ya viongozi wa vijiwe vya boda boda vilivyopo wilaya ya Monduli mjini.
ASP. Nchimbi alisema kwamba, sehemu yoyote ambayo haina utulivu katika usalama basi hakuna kinachoweza kufanyika hususani upande wa maendeleo.
" Kama kutakuwa na uhalifu uliokithiri itawakatisha tamaa wafanyabishara kufanya shughuli zao, hali ambayo itaathiri kipato chenu nyinyi (Madereva wa boda boda) maana hamtapata wateja wa kutoka kwenye Bar na kumbi nyingine za starehe hasa nyakati za usiku kwa kuwa maeneo hayo yatakuwa yamefungwa mapema kwa kuogopa uhalifu.
Vile vile watu ambao ni wateja wataogopa kutembea usiku kwa kuwa watakuwa na hofu juu ya usalama wao." Alisema ASP. Nchimbi ambaye ni mkuu wa Polisi Jamii wilaya ya Monduli.
Sambamba na hilo ASP. Nchimbi alidokeza suala la usajili wa vijiwe vyao ili wahusika waweze kutambulika badala ya Kila mmoja kukaa kijiweni kiholela Hali ambayo itawasidia kuthibitiana pindi mwenzao atafanya ndivyo sivyo.
Alisema madereva wa Boda boda ni watu muhimu katika kuimarisha usalama wilayani humo kwa kuwa huwa wanakesha mpaka asubuhi hivyo ni rahisi kwao kushuhudia matukio mbalimbali yakiwemo ya kiuhalifu na kuwezesha kutoa taarifa haraka kwa Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake mmoja wa viongozi hao wa vijiwe vya Boda boda aliyefahamika kwa jina la Teeneger Mwinyi alisema kwamba, wanatamani kuwe na mkutano baina ya Jeshi hilo na wao ili na madereva wengine wapate elimu hiyo na hatimaye kuwa kufanya kazi kwa pamoja kwa nia ya kutokomeza uhalifu.
Wilaya ya Monduli mjini ina jumla ya vijiwe 14 vya madereva wa Boda boda ambavyo vimegawanyika katika maeneo mbalimbali.

0 Comments:
Post a Comment