WAZIRI wa nchi Ofisi wa Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Arusha kusimamia utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Kikatiti mpaka Sakila wilayani Arumeru.
Amesema utekelezaji huo ulio kwenye hatua za awali za ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji ukikamilika unatarajiwa kunufaisha wananchi wa eneo hilo wanaojishughulisha na kilimo cha mboga na mazao mengine ya nafaka yanayotumiwa kwenye jiji la Arusha.
Pia amelipongeza na kulihakikishia ushirikiano Kanisa la International Evangelism Church (IEC) kwa shughuli wanazofanya kwa jamii ikiwemo miradi ya maendeleo anayotekeleza kwenye mikoa ya Arusha na Manyara katika sekta za elimu, afya, maji na maendeleo ya jamii.
Mhagama ameyasema hayo leo Desemba 2,2023 wakati akiongea kwenye mahafali ya 83 ya Chuo cha Biblia Sakila kinachotoa elimu bure ambapo jumla ya wanachuo 76 walihitimu kwa ngazi ya stashahada ya uchungaji, uinjilisha, utume, unabii na ualimu.
"Waziri Mkuu, (Majaliwa Kassim Majaliwa) alipokuja hapa mwezi juni alikuta kuna tatizo la umeme akaagiza lishughulikiwe na TANESCO limeisha na kituo hiki kimekuwa cha kimataifa kweli kama kinavyotambulika hakina shida ya umeme tena," alisema Waziri Mhagama na kuongeza.
"Suala la pili ni la barabara nimeongea na Nassari (mkuu wa wilaya ya Monduli kwenye hafla hiyo alikuwa anamwakilisha mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela) ameniambia mazao yote yanayolimwa huko milimani yanapita kwenye barabara hii yakipelekwa kulisha jiji la Arusha na maeneo mengine,".
Waziri Mhagama alisema kuwa tayari maelekezo ya Waziri Mkuu yameanza kufanyiwa kazi na TAMISEMI kwani tayari uchambuzi yakinifu umefanyika na mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami uko kwenye hatua za awali za uchimbaji wa mitaro ya kupitisha maji.
"Namwagiza Mkuu wa Mkoa ahakikishe barabara hii inapitika kipindi chote cha mwaka wakati ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ukiendelea ," aliagiza waziri Mhagama akirejea umuhimu wa barabara hiyo kwa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Sakila na vijiji vya jirani.
Aidha alimpongeza Askofu Mkuu wa IEC, Dk Elihudi Issangya kwa mpango wake wa kuanzisha Chuo Kikuu kwa kile alichoeleza kuwa mbali ya kuongeza mtandao wa vyuo vikuu nchini lakini kitasaidia kuwanoa vijana kwa kile alichosisitiza elimu ya kitaaluma na dini itasaidia kujenga jamii iliyo bora.
Waziri Mhagama alisema kuwa changamoto ya ukosefu wa gari la kubeba wagonjwa kwenye zahanati ya Sakila inayomilikiwa na kanisa hilo ameichukua ataenda kuifanyia kazi huku akimwagiza na mkuu wa mkoa wa Arusha kuichukua akaangalie yeye na timu yake ya mkoa wanavyoweza kuitatua.
Alisema kuwa amesikia pia wana Chuo cha Ufundi Stadi kinachomilikiwa na kanisa hilo hivyo ameahidi kushughulikia ili kiweze kunufaika na mpango wa Rais Samia ambao amekuwa akitoa ruzuku kwenye vyuo hivyo ili kuwezesha vijana kupatiwa bure elimu inayowawezesha kujiari.
Akimalizia waziri Mhagama aliwataka wahitimu wakawafundishe watu kwa upendo na kuwaunganisha badala ya kuwasambaratisha na wakaeneze injili yenye maadili yenye kuunganisha bila kisahau umuhimu wa kutunza mazingira.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa EIC, Askofu Issangya alimshukuri Rais Samia kwa uongozi wake bora aliodai kuwa aliuona moyo wake wa kulea jamii bora hata kabla hajashika wadhifa huo wa juu kabisa.
Alisema kuwa wamekuwa wakitoa elimu inayolenga kulinda maadili, kuheshimiana sanjari na ujenzi wa misingi wa familia bora.
Awali Makamu Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Yohane Mgonja alisema kuwa tokea chuo hicho cha biblia Sakila kianzishwe mwaka 1983 kimetoa mafunzo kwa watumishi zaidi ya elfu10 kutoka ndani na nje ya nchi ambapo kwa sasa wana malengo ya kujenga Chuo Kikuu na kuboresha zahanati ya Sakila ili ifikie hadhi ya kuwa hospitali.
Alisema kuwa IEC imejenga zahanati inayotoa huduma bure kwa jamii ya wananchi wanaoishi Sakila, chuo cha ufundi Maji ya Chai, shule ya awali, shule ya msingi SLUYS na sekondari ya Hebron yenye kutoa elimu mpaka kidato cha sita.
"Chuo hiki kimechimba maji kwenye maeneo mengi bila kudai chochote mfano kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid (Arusha), katika shule za msingi na sekondari Sinoni Unga Limitedi jijini Arusha, kituo cha walekavu Usa River na kwenye hospitali ya wilaya ya Arumeru," alisema Mgonja.
Alisema kuwa wamechimba maji kwenye eneo la Ngaramtoni na Mringaringa na kufunga mtambo wa solar hivyo wananchi wanapata maji bila shida yoyote.
Mgonja alisema kuwa Chuo kimekuwa mdau katika ujenzi wa zahanati wilayani Simanjiro na wamechimba visima vinne na kufunga mitambo ya umeme wa sola hivyo maji yanapatikana bila shida yoyote.
Kanisa hilo pia wanatoa huduma ya kusaidia wazee kwa kuwapa chakula na huduma za afya huku wakiwa na kituo cha watoto yatima ambacho huwapatia huduma zote muhimu ambapo watoto hao mbali ya chakula,mavazi, malazi na matibabua pia hupatiwa elimu kuanzia shule ya awali sekondari na chuo cha ufundi kwenye shule za kanisa hilo.
IEC pia inamiliki kituo Kituo cha radio cha New Life kinachotoa elimu kwa jamii sanjari na kueneza neno la Mungu na huduma ya maombi makanisa mengi yameanzishwa na waliohitimu katika chuo hicho.





0 Comments:
Post a Comment