ZARA AHIMIZA "TWENZETU KILELENI" NA UTUNZAJI MAZINGIRA


KAMPUNI ya Uwakala wa Utalii ya Zara Tanzania Adventures, chini ya uongozi wa Mkurugenzi Zainab Ansell, imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kulinda mazingira na utalii wa Mlima Kilimanjaro. 

Kupitia kampeni ya 'Twenzetu Kileleni Kilimanjaro,' Zainab  amewaomba Watanzania kushiriki katika madhimisho ya miaka 62 ya uhuru kwa kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika  na kushirikiana katika zoezi la kupanda miti kabla ya kupanda mlima.


Mkurugenzi huyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, akisema, 'Tukiweza kushirikiana pamoja tunaweza, tutakuwa na zoezi la kupanda miti kabla ya kupanda mlima kuonyesha kwamba tunaweza kulinda mazingira na mlima wetu.' Kwa kuongezea, wageni wa ZARA Tanzania Adventures hupanda miti kama sehemu ya utamaduni wao.


Kampeni hii inaenda sambamba na juhudi za ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na wadau wengine katika kuboresha utalii na kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro. Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu, ameipongeza kampuni hiyo kwa kushirikiana na KiliMedAir kuhakikisha usalama wa wapanda mlima ambapo inapotokea dharura ndege za uokoaji za kampuni hiyo zitatumika kuokoa .


Jumla ya watu 320 wanatarajiwa kupanda mlima mwaka huu kwa ajili ya maadhimisho hayo ambapo  ZARA Adventure itapandisha watu 200 kupitia lango na Marangu.


Awali mwanzoni mwa mwezi huu. Mkuu wa Mkoa, Kilimanjaro, Nurdin Babu  alitoa mwito kwa wananchi kushiriki katika kampeni ya 'Twenzetu Kileleni Kilimanjaro' kusherehekea miaka 62 ya uhuru wa Taifa. 

Pia, aliipongeza ZARA kwa kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti na kampeni za kuhifadhi mazingira.


Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kampeni hiyo kwa kusema, 'Tunaenda kufanya kampeni ya upandaji miti kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, hadi tarafa.' Hii ni sehemu ya jitihada za pamoja za kuhifadhi mazingira na utalii wa Mlima Kilimanjaro, ikithibitisha dhamira ya kulinda hazina hii ya asili kwa vizazi vya sasa na vijavyo."




0 Comments:

Post a Comment