WANANCHI NGORONGORO WACHARUKA, WATOA UTHIBITISHO CHUMVI YA MIFUGO WALIYOPEWA ILIKUWA NA SUMU



WANANCHI wa Tarafa ya  Ngorongoro wametoa vithibitisho vya matokeo ya maabara nne tofauti za serikali yanayoonyesha madini ya chumvi ya mifugo yaliyosambazwa na serikali 2021 yalikuwa na viambata vya sumu.


Wamewasilisha matokeo ya vipimo yaliyotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Wakala wa Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) ambayo yote yanaonyesha madini ya chumvi hayafai kwa matumizi ya mifugo.

Aidha, wananchi hao wametaka waliohusika na hujuma hiyo wawajibishwe sanjari na wafugaji kulipwa fidia ya mifugo yao iliyokufa huku wakitaka utaratibu wa awali wa kuingiza mifugo kreta kwa ajili ya kunywa maji yenye madini asilia urejeshwe kwani hawana imani na chumvi ya kupewa na serikali.

Wananchi hao wameyasema hayo, Oktoba 15, 2023, jijini Arusha wakati wakiongea na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya sakata la madini ya chumvi yaliyosambazwa na serikali kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kuibuliwa, na kuua mifugo mingi ya wafugaji hivyo kuwafanya wananchi kuwa mafukara.

Ambapo baada ya sakata hili kujitokeza, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) ilitoa taarifa ikikanusha madai ya wananchi huku wakidai kuwa hakuna utafiti wa kisayansi na kimaabara umerithibitisha hayo.

Diwani wa kata ya Ngorongoro, Simon Saitoti, ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa timu ya watu wanne iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, kupeleka madini ya chumvi hayo kufanyiwa uchunguzi anaeleza. 

Mwanakijiji wa Ngorongoro, Kasale Mwaana, akitoa ufafanuzi kuhusu jinsi madini hayo ya chumvi yalivyosababisha vifo vya mifugo na madhara kwa wale waliotumia nyama. Alidai kuwa tukio hili linaonekana kuwa na nia ovu ya kupunguza si tu idadi ya mifugo, bali pia idadi ya watu ndani ya eneo hilo. Mara nyingi, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) wamekuwa wakilalamika kwamba idadi ya watu na mifugo inaathiri shughuli za uhifadhi.

Diwani wa Misigiyo, Rokoine Moti, amemuomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati na kuwanusuru wananchi. Alidai kwamba wasaidizi wa Rais wanampotosha, huku akifafanua kuwa kwenye kata ya Ngorongoro, jumla ya mifugo 10,020 wamekufa.

Mkazi wa kijiji cha Oloirobi, Melubo Ndara Poshe, alisema hawana imani tena na NCAA kuwaletea chumvi nyingine.

Mwenyekiti wa kijiji cha Oloirobi, Mbarnot, alisema ni vema serikali kuruhusu mifugo kunywa maji ya madini kreta, kwani hawana imani na madini watakayopewa na serikali, kama hayataua mifugo yao tena.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mokilal, Thomas Marite, alielezea jinsi walivyokuwa wakiwapa mifugo chumvi hiyo. Alidai kwamba kumekuwa na propaganda inayoelezwa kwamba wananchi wa Ngorongoro wote wamehamia Msomera, jambo ambalo si kweli.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kayapus, Osoi Naitwat, alisema jumla ya mifugo 6,294 ilikufa kwenye kijiji chake. Alisisitiza kwamba adhari ya sumu hiyo haikuwa kwa mifugo pekee, bali pia kwa binadamu waliokunywa maziwa na nyama. Tayari watu kadhaa wamekufa na wengine wako hospitalini wakisumbuliwa na magonjwa ya ini.

Haya ni matukio yanayowasilishwa na wananchi wenyewe, wakihoji uhalali wa hatua zilizochukuliwa na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro. Wametoa wito kwa serikali kuchunguza kwa kina suala hili na kuchukua hatua za haraka kurejesha imani ya wananchi. Kwa sasa, jamii ya Ngorongoro inakabiliana na changamoto kubwa ya kupoteza mifugo yao na hata vifo vya binadamu kutokana na madhara ya madini hayo.

Juhudi za kumpata Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya jumatatu Oktoba 16,2023, kuongea na mwandishi wa habari hizi aliahidi kutolea ufafanuzi suala hilo akimaliza kikao cha ulinzi na usalama.

Hata hivyo hakufanya hivyo na alipopigiwa simu leo junanne Oktoba 16,2023 hakupokea simu hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake pia hakujibu.


Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Kitengo cha Uhusiano wa Umma, NCAA,  Kassim Nyaki alipoulizwa juu ya madai hayo ya wananchi wa tarafa ya Ngorongoro alisema kuwa tayari walishatolea ufafanuzi suala hiyo kwenye taarifa yao kwa umma waliyoitoa Oktoba 7,2023.










0 Comments:

Post a Comment