Serikali Yatataka Ushirikiano Zaidi Kukuza Sekta ya Maziwa Nchini

 


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dr. Fabian Madele, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya maziwa nchini Tanzania kuimarisha ushirikiano ili kuongeza tija katika uzalishaji, usindikaji, na masoko ya maziwa. 

Hatua hiyo inalenga kuongeza kipato cha wafugaji na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.



Dr. Madele aliyasema hayo alipotembelea banda la maonesho la shirika la Heifer International Tanzania wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ya Kitaifa yanayofanyika mkoani Iringa.
Katika ziara hiyo, alijionea jinsi Heifer Tanzania inavyoshirikiana na serikali pamoja na wadau wengine katika kukabiliana na njaa na umaskini kupitia mbinu bora za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo.
Heifer Tanzania ilionyesha mafanikio ya miradi yake mbalimbali inayowasaidia wafugaji wadogo wa maziwa kuongeza uzalishaji, kupata masoko ya uhakika, na kuboresha maisha ya familia zao. Aidha, shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa maziwa kupitia mafunzo, uwezeshaji wa kifedha, na uimarishaji wa vikundi vya ushirika.

Dr. Madele alilipongeza shirika la Heifer Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya maziwa. Alisisitiza kuwa ushirikiano thabiti kati ya Serikali, sekta binafsi, na washirika wa maendeleo ni nguzo muhimu katika kufikia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu: “Boresha Biashara ya Maziwa, Linda Afya ya Mlaji, Ongeza Kipato na Changia Ukuaji wa Ochumi.”

Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa ya Kitaifa yanafanyika mkoani Iringa kuanzia tarehe 28 Mei hadi 1 Juni, yakikutanisha wadau wakuu kutoka sekta nzima ya maziwa kujadili fursa, changamoto, na mikakati ya kukuza uzalishaji, unywaji wa maziwa, na maendeleo ya masoko nchini Tanzania.


0 Comments:

Post a Comment