Mradi wa TI3P Wanufaisha Zaidi ya Wadau wa Maziwa 92,000 Tanzania, Zaidi ya Bilioni 42 SGR Zasimamiwa


 Jumla ya wafugaji wa ng'ombe wa maziwa na wadau wa mnyororo wa thamani 92,831 (asilimia 30 wakiwa wanawake) kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamefaidika na Mradi wa Ushirikiano Jumuishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P). Mafanikio hayo yamefikiwa tangu kuzinduliwa kwa mradi huo mnamo Machi 2022.

Mradi huu unafadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Taasisi ya Bill & Melinda Gates. Unatekelezwa kwa ushirikiano na mashirika ya Heifer International, Land O’Lakes Venture37, na Tanager. Lengo kuu ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza tija, na kuboresha kipato cha wafugaji wadogo.

Uwekezaji na Miundombinu

Tangu kuanza kwake, mradi umefanikisha utoaji wa mikopo na ufadhili wa zaidi ya shilingi bilioni 42 kwa wasindikaji, wakulima, wasambazaji wa pembejeo, na wadau wengine. Fedha hizo zimesaidia:
  • Kuanzishwa kwa viwanda vipya vya kusindika maziwa.
  • Upanuzi na uboreshaji wa viwanda 17 vilivyopo kwa uwekezaji wa bilioni 22.8.
  • Ununuzi wa mitamba bora ya maziwa 3,330 yenye thamani ya zaidi ya bilioni 11.09, hatua iliyoongeza uzalishaji wa maziwa nchini.

Huduma za Ugani na Uwezeshaji Viwanda

Mradi umeongeza upatikanaji wa huduma za ugani, pembejeo bora, masoko, na fursa za kifedha. Jumla ya viwanda 19 vya maziwa vimeshiriki katika programu za kukuza biashara (Enterprise Acceleration Interventions) ili kuongeza ufanisi wa utendaji, faida, na matumizi ya uwezo wa viwanda hivyo kusindika maziwa.

Kukuza Usawa wa Jinsia

Katika kuleta ukuaji jumuishi, TADB ilitoa ruzuku za ulinganifu (matching grants) za shilingi bilioni 1.4 kwa wafugaji wadogo 1,216, wakiwemo wanawake 397. Hatua hii imepunguza vikwazo vya kupata mikopo ya mitamba na kupanua uwekezaji.
Aidha, viwanda vitano vya maziwa vinavyomilikiwa na wanawake vilipokea vifaa vya kupatisha maziwa (pasteurization equipment) vyenye thamani ya shilingi milioni 75. Wanawake wengine watano wasindikaji walipokea ruzuku za TI3P, huku wasindikaji 12 wakipata ruzuku maalum za kukuza usawa wa jinsia katika biashara zao.

Ukusanyaji na Ubora wa Maziwa

Ili kuboresha mifumo ya ukusanyaji na ubora wa maziwa, mradi umeanzisha na kuimarisha Vikundi vya Wakulima (FPOs) 45 na Vikundi vya Wadau wa Maziwa. Vikundi hivi sasa vinakusanya zaidi ya lita 25,664 za maziwa kila siku, hatua inayoshirikisha masoko vizuri na kuongeza nguvu ya wakulima kupanga bei.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Maziwa mkoani Iringa, Kuratibu wa Mradi wa TI3P, Joseph Mabula, alisema mradi umefanikisha ujenzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa nchini kwa gharama ya uwekezaji ya shilingi bilioni 1.157. Utekelezaji huo ulifanyika kwa ushirikiano na wasindikaji, vyama vya ushirika, na washirika wa mradi.
Mabula alibainisha kuwa mradi huo pia unashughulikia changamoto za kisera na kisheria zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo. Unasisitiza pia masuala ya mtambuka kama usawa wa kijinsia na lishe ili kuhakikisha maendeleo endelevu. Alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto za tasnia ya maziwa na kutumia kikamilifu fursa zilizopo.

0 Comments:

Post a Comment