WANANCHI JITOKEZENI UZINDUZI JENGO LA PAPU-MONGELA



MKUU wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema uwepo wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika, (PAPU Tower) jijini Arusha moja ya ongezeko la vivutio vilivyopo mkoani hapa kutokana na ukweli kuwa ndiyo jengo refu kiliko yote yaliyomo kwenye jiji hilo kwa sasa.

Aidha amewaomba wananchi kujitokeza kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa jengo hilo kesho Septemba  2, 2023.



Ameyasema hayo leo Septemba mosi,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi  ya uzinduzi wa jengo hilo lilipo maeneo ya Philips.

Mongella amesema serikali  imejipambanua katika kuleta  mageuzi makubwa katika kusukuma uchumi wa nchi kwa kuboresha  sekta zote ikiwemo ya mawasiliano ambapo  Shirika la Posta nchini limeboresha utoaji wa  huduma zake  na linaenda kidijitali.

"Uwepo wa jengo hili Arusha ni fahari kwa nchi yetu kwani inatuongezea  utalii mwingine, uzuri wake unavuta watu mbalimbali kuja kuliangalia, niwaombe wananchi tuje kuungana na kipenzi chetu Rais Samia kulizindua jengo hili," amesisitiza Mongela..


Kwa upande wake, Mkuu wa shirika la Posta nchini,  Macrice Mbodo amesema kuwa katika wanatoa huduma kwa urahisi na kisasa bila kumuingiza mteja hasara wanatoa huduma kwa kutumia vifaa vya kisasa yakiwemo magari, pikipiki na vingine .
 

"Kama sasa tunamagari ambayo tunasafirisha samaki kutoka Mwanza hadi Uganda wakiwa salama, lakini parachichi inasafirishwa kutoka Njombe hadi mkoani Mwanza yakiwa katika ubora wake,hii yote kazi ya serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta hii na kuwa ya kidijitali," amesema Mbodo.



Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kuwa kabla ya uzinduzi wa jengo hilo watoa huduma za posta wamepata  fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali ambayo yamelenga kuimarisha misingi imara ya utoaji  huduma za posta zitaendelea kustawi hivyo kuchangia maendeleo ya mataifa yao.

Amepongeza  uamuzi uliofanywa kuandaa mkutano wa mawaziri uliowawezesha kubadilishana uzoefu na kutafakari juu ya jukumu ambalo Huduma za Posta katika nchi zao zinaweza kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kwa kuchangia maendeleo endelevu.

Awali viongozi Agosti 31,2023 walikagua jengo hilo linalovutia kwa muonekano wake kwani mbali ya kuwa jengo refu kuliko majengo mengine yaliyopo jijijini Arusha kwani lina ghorofa 18 lakini pia lina muonekano mzuri wa kuvutia kutokana na namna lilivyojengwa.

0 Comments:

Post a Comment