KESI ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imekwama kuendelea kusikilizwa baada ya hakimu anayeisikiliza, Patricia Kisinda kuwa na majukumu mengine ya kiofisi.
Pamoja na mambo mengine mahakama hiyo ilipanga kutoa uamuzi mdogo juu ya maombi ya mshitakiwa wa tatu, Watson Mwahomange aliyeiomba itoa amri kwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU) impatie simu yake ya kiganjani ili aweze kuitumia kujitetea.
Akiahirisha kesi hiyo, Leo Alhamisi Machi 10, 2022, Hakimu Mkazi Pamela Meena alieleza kuwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kisinda, anayesikiliza shauri hilo bado anaendelea na majukumu ya kiofisi hataweza kuendelea kulisikiliza hadi Jumatatu Machi 14, 2022.
"Hakimu bado anaendelea na majukumu ya kiofisi hataweza kuendelea kusikiliza shauri hili kwa hiyo kesi itaendelea kusikilizwa Jumatatu,"amesema Meena.
Mwahomange, ambaye alishindwa kujitetea jana baada ya mawakili wanaowatetea washitakiwa wengine kuweka pingamizi kuzuia mahakama kutoa amri kwa Takukuru kumpatia simu yake aitumie kujitetea.
Aidha mbali na uamuzi huo mdogo, pia shahidi wa tano wa utetezi ambaye pia ni mshitakiwa wa sita, Jackson Macha (30) alikuwa anaendelea kujitetea kwa siku ya pili .
0 Comments:
Post a Comment