KESHO Oktoba 15, 2021 mahakama ya hakimu mkazi Arusha inatarajiwa kutoa uamuzi kwenye kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili.
Awali uamuzi huo ulipangwa kutolewa Oktoba mosi, mwaka huu lakini ulishindikana kutolewa kwakuwa haukuwa umekamilika.
Siku hiyo Oktoba 1, 2021 shauri hilo linalofuatiliwa na wengi liliahirishwa na hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Arusha, Amalia Mushi.
Alisema kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya maamuzi lakini maamuzi hayo hayajakamilika kuandaliwa hivyo ameahirisha shauri hilo mpaka Oktoba 15, mwaka huu kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Kwa mujibu wa sheria ya kanuni ya adhabu ya makosa ya jinai endapo washitakiwa hao watakutwa na hatia adhabu ya juu ni kifungo cha maisha na adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.
Awali wakili wa serikali mwandamizi, Tarsila Gervas ameieleza mahakama hiyo kuwa shauri lilikuwa limepangwa kwa ajili ya hukumu na upande wa Jamhuri wako tayari kusikiliza hukumu ya mahakama.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi Dancan Oola amesema yeye na mawakili wenzake wako tayari tayari kupokea hukumu ya mahakama.
Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni Silvester Nyegu na Daniel Mbura.
Awali Agosti 24, mwaka huu, hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo anayesikiliza shauri hilo la jinai namba 105/2021 kwenye mahakama ya hakimu mkazi Arusha alipanga kutoa uamuzi Oktoba mosi mwaka huu.
Aliwaeleza mawakili wa pande zote, Jamhuri na utetezi wanatakiwa kuwasilisha hoja zao za majumuisho kwa maandishi ndani ya wiki moja kuanzia siku hiyo mpaka Septemba mosi, mwaka huu.
Hakimu Odira alitoa maelekezo hayo baada ya mawakili wa utetezi Duncan Oola, Moses Mahuna, Silvester Kahunduka Freedolin Gwemelo kuiomba mahakama kufunga utetezi kwani hawana mashahidi wengine .
Kwa upande wake wakili wa serikali mkuu, Tumaini Kweka aliieleza mahakama kuwa kila kitu kwa upande wa Jamhuri wao walishafunga kila kitu.
Awali shauri hilo lililoanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Julai 19, mwaka huu upande wa jamhuri ulileta mashahidi 11 na vielelezo nane huku upande wa utetezi kila mshitakiwa akijitetea mwenyewe wakiwa na vielelezo vitatu.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 9, mwaka huu kwenye duka la Shaahid stores lililopo mtaa wa bondeni kata ya Kati jijini Arusha.

0 Comments:
Post a Comment