ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), kwa
tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Antony Komu,
ameibwaga Serikali kwenye kesi aliyoifungua mahakama ya Afrika
Mashariki, (EACJ) baada ya maombi yake mawili kukubaliwa huku moja
likitupwa.
Mahakama hiyo imesema kuwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania lilikiuka kipengele cha 50 (1) cha uanzishwa wa jumuiya ya
Afrika Mashariki kwenye uchaguzi uliofanyika Aprili 17, 2012.
Uamuzi huo wa shauri hilo namba 7/ 2012 la kutaka tafsiri ya kipengele
hicho, ulitolewa jana na Jaji Mkuu wa mahakama hiyo, Jean Bosco Butasi
kwa saa 1:20 kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 4:20 asubuhi kwenye
mahakama hiyo iliyopo jengo la makao makuu ya EAC, Arusha.
Alisema kuwa kitendo cha Bunge la Tanzania kutengeneza makundi manne
ya wagombea kwa kigezo cha jinsia, Zanzibar, vyama vya upinzani na
Tanzania Bara ambayo wagombea wote walitokana na vyama vya siasa
ulikinzana na kanuni ya 50 (1) ya mkataba wa uanzishwaji wa EAC
inayotaka kuwe na ushiriki wa makundi mbalimbali ya jamii.
Jaji huyo alisema kuwa, pia kuruhusu mgombea kutoka chama cha siasa
cha TADEA, Lifa Chipaka kushiriki uchaguzi huo kutoka kundi la vyama
vya siasa wakati chama hicho kikiwa hakina uwakilishi bungeni ni
kinyume na kipengele hicho cha mkataba huku akishauri kuwa angeweza
kugombea kupitia makundi mengine ndani ya jamii.
Aidha mahakama hiyo ililionya bunge hilo kuhakikisha katika chaguzi
zake zinazofuata kuwa makini kuhakikisha mkanganyiko wa aina hiyo
haujirudii.
"Suala la kama wabunge wanaoiwakilisha Tanzania kwenye EALA
wamechaguliwa kihalali au hapana litaamuliwa na mahakama Kuu ya
Tanzania," alisema Jaji huyo wakati akisoma uamuzi huo.
Aidha aliuagiza upande wa wajibu maombi, Mwansheria Mkuu wa Serikali
kumlipa mleta maombi, Komu robo ya gharama alizotumia kwenye shauri
hilo.
Hata hivyo mahakama hiyo ilitupa ombi moja lililowasilishwa mahakamani
hapo na Komu akitaka kwa kuwa Chadema ni chama kikuu cha upinzani
kilipaswa kupata nafasi kwenye bunge la EALA badala ya nafasi hiyo
kupewa vyama vyenye idadi ndogo ya uwakilishi wa wabunge.
Kwa upande wake mawakili wa Komu, Edson Mbogoro na John Mallya
walisema wamerikidhika kwa uamuzi huo huku wakisema kuwa sasa
wanajielekeza kwenye shauri walilolifungua kwenye mahakama kuu kanda
ya Dodoma.
Mallya alisema kuwa kwenye shauri hilo namba 1/2012 litakalorudi
mahakakani hapo kwa ajili ya kupanga tarehe za kuendelea na
usikilizwaji novemba 27,mwaka huu wanaiomba mahakama hiyo itengue
matokeo ya uchaguzi wa wabunge wa EALA kutokana na ukiukaji wa kanuni
ikiwemo kipengele cha 50 (1) cha mkataba wa uanzishwaji wa EAC.
Kwa upande wake wakili wa Serikali, Nkasari Sarakikya, alisema kuwa
wanasubiri kupata nakala ya uamuzi huo waupitie ndipo waweze kujua
nini cha kufanya ambapo alishirikiana na mawakili Pius Mboya na Mark
Mukwamo.
SERIKALI YATOA TAKRIBANI SHILINGI BIL. 41 KUBORESHA MIONDO MBINU SUA
-
NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Takribani shilingi bilioni 41 zimetolewa na serikali kupitia Mradi wa Elimu
ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa...
8 hours ago
0 Comments:
Post a Comment