![]() |
| Mkurugenzi wa jiji la Arusha,Juma Iddi akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali za madiwani wa jiji la Arusha. |
![]() |
| Diwani wa kata ya Sombetini, Ally Bananga, (CHADEMA) akichangia hoja kwenye kikao cha baraza |
waandishi wa habari wakiwa wamekaa mbele ya madiwani wakati wa kikao cha baraza la madiwani
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wameagiza
kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria aliyekuwa Daktari wa Jiji
hilo,Ibrahim Isack kwa tuhuma za kujimilikisha vifaa vya zahanati
ya Levelosi.
Aidha wameagiza kukamilishwa mara moja kwa wataratibu za
kumwezesha aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa jiji, Estomih Chang’a, ambaye sasa ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpanda, ili afike kutoa maelezo ya juu ya
upotevu vifaa hivyo.
Akiongea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani jana, Diwani
wa kata ya levelos, Ephata nanyaro, (CHADEMA), alisema kuwa hakubaliani na
majibu ya Mkurugenzi wa Jiji, Juma Iddi kuwa suala hilo liendelee
kushighulikiwa kwenye kamati ya fedha kwani suala hilo limekuwa
likishughulikiwa kwa miaka mitatu sasa bila kupata ufumbuzi.
“Mimi nina ushahidi, kwanza nilimuona Dkt Ibrahim akipakia vile vifaa kwenye lori,
pili nilifuatilia KCMC wakanipa barua kuonyesha hawakuchukua vile vifaa hata
wale Wamarekani waliofadhili mradi huo,
(Familly Health International) wamenitumia barua pepe hawakuchukua vile vitu.
“Sasa tutakuwa tunajadili nini wakati huu ni wizi, hii ni
jinai wanatakiwa wakamatwe wafikishwe polisi,” alisema Nanyaro wakati akijadili
taarifa za utekelezaji zilizokuwa zikiwasilishwa.
Akiongea na waandishi wa habari Nanyaro alisema kuwa
vifaa hivyo vilikuwa vikitumiwa na KCMC kwa ajili ya kutafiti magonjwa ambukizi
ikiwemo HIV ambapo mradi huo ulikuwa ukifadhiliwa na FHI, ambapo waliomba eneo
kwa Halamshauri ya jiji kwa makubaliano kuwa mradi huo ukikamilika wataacha
vifaa.
Nanyaro alisema kuwa halmashauri waliwapa eneo kwenye
eneo la zahanati ya levelos ambapo mradi
huo ulianza 2008 na kukamilika julai, 2012 jambo alilodai kuwa baada ya hapo Dkt Ibrahim aliamua kujitwalia vifaa hivyo kwa
maelezo kuwa KCMC walivichukua wakati si kweli.
Alisema kuwa vitu hivyo ni vingi ingawa hakuwa anajua
thamani yake ambapo alitaja baadhi kuwa ni pamoja na magari mawili, samani za
ofisi, vifaa na samani za maabara huku
akidai Jenereta aliinusuru kwa yeye binafsi kuamua kuweka makufuli manne.
“Hapa wanadai kuwa Dkt Ibrahim hapatikani kupitia namba
ya simu aliyowapa, mimi ninaweza
kuwaonyesha mahali alipo hata sasa kwani yuko hapahapa mjini, hata asubuhi
nimemuona, wasipomkamata nitahamasisha wananchi wangu tumkamate tumepeleke
polisi, Mkurugenzi akapeleke tuhuma zake,” alisisitiza Nanyaro.
Awali Mkurugenzi, Iddi alilieleza baraza hilo kuwa wanasubiri majibu ya barua waliyomwandikia
Katibu Mkuu wa TAMISEMI waliyomuomba amwagize mtumishi wake Chang’a kuja
kujieleza mbele ya baraza la madiwani.
Alisema kuwa Dkt. Ibrahim alifika kwa ajili ya kujieleza
kwenye baraza hilo Mei 15,mwaka huu lakini kikao hakikufanyika hivyo akaacha
namba ya simu ambayo kwa siku nne mfululizo wamekuwa wakimpigia hawampati.
“Tatizo kwa sasa ni kuwa kule Ngorongoro, Dkt, Ibrahim
kasimamishwa kazi kutokana na masuala mengine yanayofanana na haya
mnayomtafutia, hivyo hata muajiri wake inamuia vigumu kumpata, inawezekana
ameamua kuzima simu kabisa baada ya tume iliyokuwa ikimchunguza kuja kutuhoji
na huku kuhusu masuala haya ila
tunaendelea kumtafuta,” alisema Iddi.
Alimtaka diwani, Nanyaro kuwakabidhi vielelezo
alivyonavyo ili waone namna watakavyoweza kumchukulia hatua za kisheria Dkt
Ibrahim baada ya mwanasheria wa jiji kuvifanyia kazi.



0 Comments:
Post a Comment