Watu 14 Wafariki, Wengine Kadhaa Wajeruhiwa Vibaya Katika Moto wa Kiwanda Korea Kusini

 


Watu 14 wamepoteza maisha huku wengine 25 wakijeruhiwa vibaya kufuatia moto mkubwa ulioteketeza kiwanda cha kutengeneza vipuri vya magari katika mji wa Daejeon, Korea Kusini.

Kwa mujibu wa mamlaka za usalama, moto huo ulizuka majira ya mchana siku ya Ijumaa wakati wafanyakazi wakiwa kwenye mapumziko ya chakula. Juhudi za kuudhibiti zilifanikiwa kufikia saa 5:48 usiku. Aidha, watu wengine 35 waliripotiwa kupata majeraha madogo katika tukio hilo.

Kiwanda hicho kinamilikiwa na kampuni ya Anjun Industrial, ambayo huzalisha vifaa vya injini kwa ajili ya makampuni makubwa ya magari yakiwemo Hyundai Motor na Kia Corp, kwa mujibu wa taarifa za kampuni hiyo.

Kupitia taarifa rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Sohn Ju-hwan, aliomba radhi kwa tukio hilo na kueleza kuwa kampuni itashirikiana kikamilifu na mamlaka kuchunguza chanzo cha moto huo. Pia aliahidi kufanyika kwa tathmini ya kina ya mifumo ya usalama na utekelezaji wa hatua madhubuti za kuzuia ajali kama hiyo kutokea tena.

Serikali ya Korea Kusini iliunda kikosi maalum cha kukabiliana na majanga kikijumuisha idara mbalimbali, kufuatia agizo la Rais Lee Jae Myung la kutumia rasilimali zote zilizopo kudhibiti moto huo na kuokoa maisha ya watu.

0 Comments:

Post a Comment