Thamani ya Mtu Ipo Kwenye Vipawa na Talanta – Makonda



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesisitiza kuwa thamani ya mtu haipaswi kupimwa kwa nafasi aliyonayo, kazi yake, dini au kabila lake, bali inatokana na vipawa na talanta alizowekewa na Mungu.



Akizungumza katika kikao kazi cha Maafisa Michezo kilichofanyika katika Arusha International Conference Centre (AICC), jijini Arusha, Waziri Makonda alieleza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika sekta za utamaduni, sanaa na michezo kama nyenzo muhimu ya kukuza vipaji vya Watanzania.

Alibainisha kuwa sekta hizo zina mchango mkubwa katika kujenga heshima ya taifa, kukuza ubunifu, pamoja na kuongeza ajira kwa vijana. Hivyo, alihimiza kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kutambua na kuendeleza vipaji vilivyopo nchini.

Aidha, Waziri Makonda aliwataka watumishi wa sekta ya michezo kufanya kazi kwa weledi na viwango vya juu, kulinda heshima ya ofisi zao, na kutumia nafasi walizonazo kuhakikisha wanabaini na kukuza vipaji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kauli ya Waziri Makonda ni wito kwa jamii nzima kutambua kuwa kila mtu ana thamani ya kipekee inayotokana na vipawa vyake. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuvibaini, kuvikuza, na kuvitumia kwa maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.


0 Comments:

Post a Comment