Tanzania Yazindua Jengo la Makao Makuu ya Mahakama, la Kwanza kwa Ukubwa Afrika na la Sita Duniani

 


Tanzania imeandika historia mpya kwa kuzindua jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama, ambalo linatajwa kuwa la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la sita duniani. 



Hafla hiyo ya kihistoria ilifanyika tarehe 5 Aprili 2025, katika eneo la Tambukareli, Jijini Dodoma, na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mahakama, na wadau wa sekta ya sheria nchini.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliongoza uzinduzi wa jengo hilo pamoja na majengo mengine ya muhimu, ikiwa ni pamoja na Jengo la Utumishi wa Mahakama na Makazi ya Majaji. 



Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alieleza furaha yake kutokana na juhudi zilizofanywa katika ujenzi wa jengo hilo ambalo linatoa hadhi na heshima kwa Taifa.


"Nimejionea kazi kubwa iliyofanyika, hakika jengo hili lina kila sifa ya kuitwa jengo kuu la mahakama ya Tanzania," alisema Rais Samia. "Baada ya Kazakhstan, Tanzania ni ya pili kuwa na chumba cha judiciary," aliongeza.



Rais Samia Suluhu Hassan alikiri kwamba jengo hili ni urithi wa kipekee unaolenga kuboresha utoaji wa haki nchini. Alisema kuwa hatua hii inaongeza fursa za kiuchumi na kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi, na pia ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mifumo ya sheria na utawala bora inaboreshwa.


Akizungumzia mchango wa washirika wa maendeleo, Rais Samia alishukuru mataifa wahisani, akitaja Benki ya Dunia kama miongoni mwa waliotoa msaada wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili. Alisisitiza kwamba uzinduzi wa jengo hili ni sehemu ya mchakato wa kuhamia Dodoma kwa serikali, na kwamba ni hatua kubwa katika kuimarisha muhimili wa mahakama nchini.


Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, alieleza kwamba uzinduzi wa majengo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita kuimarisha taasisi za sheria. 


Alisema kuwa majengo haya yatasaidia kuboresha ufanisi na uwajibikaji wa watumishi wa mahakama, huku yakionyesha dhamira ya dhati ya Serikali kuimarisha utawala wa sheria.


"Uzinduzi wa majengo haya ni hatua kubwa katika maboresho ya mfumo wa utoaji haki na ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha taasisi za sheria nchini," alisema Waziri Ndumbaro.


Mchakato wa ujenzi wa jengo hili umeonekana kama sehemu muhimu ya mafanikio ya Serikali, kwani linalenga kuboresha ustawi wa majaji na mazingira ya kazi kwa watumishi wa mahakama. 


Hali hiyo inajenga matumaini kuwa Tanzania itakuwa na mfumo bora wa utoaji haki ambao utaongeza imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria.


Hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ilijaa shamrashamra, huku wananchi wa Dodoma wakijitokeza kushuhudia tukio hili la kihistoria. 


Uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi uliongeza uzito wa hafla hiyo, ikiwa ni ishara ya kuendelea kuimarisha mhimili wa Mahakama kama nguzo muhimu ya utawala bora nchini.


Hatua hii ya kihistoria inaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha utawala bora na kutoa huduma bora za kimahakama kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha mifumo ya sheria nchini Tanzania.

0 Comments:

Post a Comment