WAZIRI TAMISEMI AKOSHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO JIJINI ARUSHA



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, ameonesha kuridhishwa na kasi, ubora na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Jiji la Arusha, akisisitiza kuwa miradi hiyo inapaswa kukamilika kwa wakati bila kuongezewa muda.



Akizungumza jijini Arusha leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Arusha, Waziri Shemdoe amesema ziara hiyo imelenga kukagua na kutathmini utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) pamoja na miradi mingine ya maendeleo ya Jiji la Arusha.

Katika ziara hiyo, Waziri alitembelea na kukagua ujenzi wa Soko la Kilombero, uwanja wa mpira, Soko la Morombo, jengo la Utawala la Jiji la Arusha pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi kinachojengwa Bondeni City. Miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa jiji.

Waziri Shemdoe amesema miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30 inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Arusha.

Amesema kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo inaonesha usimamizi mzuri na uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa Jiji la Arusha, hali inayochangia matumizi bora ya fedha za umma na kukamilika kwa miradi kwa viwango vinavyokubalika.

Aidha, Waziri Shemdoe ameuagiza uongozi wa Jiji la Arusha kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwepo awali katika Soko la Kilombero wanapewa kipaumbele mara baada ya soko hilo kukamilika, huku akisisitiza uwazi na haki katika zoezi la ugawaji wa vizimba.



Ameonya dhidi ya vitendo vya baadhi ya watendaji au viongozi kuchukua vizimba na kuvikodisha kwa wananchi kwa maslahi binafsi, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maelekezo hayo.



Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Matle Iranghe, amesema jiji litaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia malengo ya Serikali na matarajio ya wananchi.

Meya Iranghe ameishukuru Serikali Kuu na Wizara ya TAMISEMI kwa ufuatiliaji na ushirikiano unaoendelea, akisisitiza kuwa miradi hiyo itachangia kuongeza ajira, mapato ya jiji na kuboresha maisha ya wakazi wa Jiji la Arusha.

0 Comments:

Post a Comment