MAWAKALA WA FORODHA NAMANGA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA TANCIS



MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imetoa mafunzo kwa Mawakala wa Forodha waliopo Mpaka wa Namanga, wilayani Longido mkoani Arusha, kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa maombi ya vibali vya kuingiza na kutoa mazao nchini kupitia Dirisha Moja la Mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS), uliounganishwa kutoka mfumo wa awali wa e-Kilimo.



Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Disemba 18, 2025 Namanga wilayani Longido, Afisa Kilimo wa COPRA Kanda ya Kaskazini, 

 Peter Kabelelo, alisema kuwa katika kuboresha utoaji wa huduma za vibali, Wizara ya Kilimo imeunganisha Mfumo wa e-Kilimo na Mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ili mifumo hiyo iweze kusomana.


Alisema lengo la hatua hiyo ni kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za vibali ambazo hapo awali zilikuwa zikiombwa kupitia mfumo wa e-Kilimo. Alifafanua kuwa hapo awali mteja alihitajika kutumia mifumo mbalimbali kutoka taasisi tofauti ili kupata huduma moja, kama vile COPRA, TPHPA na TANCIS.


“Maboresho yaliyofanyika yamewezesha kuunganishwa kwa mifumo hiyo ili mteja atumie mfumo mmoja tu wa TANCIS kupata huduma kutoka taasisi mbalimbali kama COPRA, hivyo kurahisisha zaidi utoaji wa huduma,” alisema Kabelelo.

Aliongeza kuwa faida nyingine ya matumizi ya mfumo huo ni kupatikana kwa takwimu sahihi za mazao yote yanayosafirishwa nje au kuingia nchini, pamoja na kujua thamani ya mazao hayo kwa usahihi.


Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Rajabu Mmunda, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kusikiliza maoni na changamoto za Mawakala wa Forodha kuhusu matumizi ya mfumo wa TANCIS.


Aliwashukuru mawakala hao kwa kushiriki mafunzo hayo na kueleza kuwa changamoto walizozitaja zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha mfumo huo unawarahisishia utendaji wa kazi kama ilivyokusudiwa na Serikali.


Naye Wakala wa Forodha wa Kampuni ya A & ED Co. Ltd, Bw. Robynson Masai, aliishukuru COPRA kwa kuwapatia elimu hiyo, akisema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kuufahamu vizuri mfumo wa TANCIS na namna unavyofanya kazi.


Hata hivyo, aliomba COPRA kuendelea kuwa karibu na mawakala hao ili kusaidia kutatua changamoto za kimfumo pindi zinapojitokeza na wanapohitaji msaada wa haraka.


Aidha, Wakala wa Forodha wa Kampuni ya Njechele Co. Ltd, Petro Mveyange, aliomba COPRA kufungua ofisi katika Mpaka wa Namanga ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa maombi ya vibali.

0 Comments:

Post a Comment