Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), leo Novemba 27, 2025 alifanya ziara maalum katika Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jijini Arusha, ambapo alikagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hii muhimu. Katika ziara hiyo, Waziri Kijaji alisisitiza kuwa uhifadhi ni msingi wa uhai, uchumi, na fahari ya Taifa letu.
Waziri Kijaji pia aliweka wazi kuwa ni muhimu kwa wananchi kushirikishwa katika ulinzi wa rasilimali za taifa, kwa kuwa wao ndio walinzi wa awali katika kuhakikisha rasilimali zinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Aliendelea kusema:
“Tunahimizana sisi Tanzania kuwa namba moja katika utalii Afrika na duniani, tuna misingi yote ya kuwa namba moja ndani ya Afrika na dunia.”
Katika ziara hiyo, Waziri Kijaji aliielekeza Menejimenti ya TANAPA kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza chachu ya utoaji wa huduma bora kwa wageni na ulinzi wa rasilimali.
Alisema lengo la Serikali ni kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030, na kwamba taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kama TANAPA, zinajukumu kubwa kuhakikisha malengo haya yanafikiwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande (Mb), alisisitiza kuwa uhifadhi ni heshima ya taifa, na kwamba maafisa na askari wa uhifadhi wana wajibu wa kulinda rasilimali za taifa kwa wivu mkubwa, masaa 24.
Alisema kuwa ni muhimu kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii ili kuhakikisha watalii wanapata huduma bora na kuhamasisha utalii wa ndani na nje ya nchi.
Kamishina wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Nassoro Kuji, alieleza kuwa ujio wa Waziri ni chachu ya kuimarisha juhudi za uhifadhi na kwamba TANAPA itaendelea kutumia teknolojia na mbinu za kisasa kulinda bioanuai na kuboresha mifumo ya ulinzi wa wanyamapori.
Ziara hiyo ilijumuisha pia hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, ambapo viongozi walipata wasaa wa kujionea vivutio vilivyopo na shughuli za utalii zinazofanywa katika hifadhi hiyo.






0 Comments:
Post a Comment