Falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo ni Reconciliation (Maridhiano), Reforms (Mageuzi), Rebuilding (Ujenzi Upya) na Resilience (Ustahimilivu), imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali nchini, hususan katika sekta ya madini kupitia ushirikiano wa serikali na kampuni binafsi kama Barrick.
Akizungumza katika kilele cha Mkutano wa Tatu wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma, Meneja wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido, alisema falsafa hiyo imekuwa dira ya mabadiliko makubwa ndani ya kampuni hiyo kwa kushirikiana na serikali kupitia ubia wa kampuni ya Twiga Minerals Corporation.
“Tumeona wajibu wetu kusapoti event hii kwa kufuata zile falsafa za 4R za Rais Samia Suluhu Hassan. Tumeziona 4R kama mfumo wa kimageuzi, na sisi kwa upande wa Barrick pamoja na Twiga zimekuwa zikiongoza utendaji wetu,” alisema Dk. Ngido.
Akielezea hatua ya kwanza ya Reconciliation (Maridhiano), Dk. Ngido alisema kampuni ilianza kwa kujenga uaminifu na kusuluhisha changamoto kati ya kampuni na jamii zinazozunguka migodi.
“Upande wa migodi ya Barrick tunakumbuka historia kilivyokuwepo. Hivyo Barrick walipochukua migodi mwaka 2019 tuliwekeza zaidi katika kuponya majeraha na kujenga uaminifu. Tulisuluhisha matatizo mbalimbali ya jamii ili kuileta kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi,” alieleza.
Katika hatua ya Reforms (Mageuzi), Barrick ilifanya mageuzi ya kiutawala kwa kushirikiana na serikali kwa kuweka uwazi na ushirikishwaji katika bodi.
“Tuliboresha utawala, tukaweka uwazi. Kwenye bodi kuna mwakilishi wa serikali na kila robo mwaka tumekuwa tukitoa taarifa kwa umma juu ya mwenendo wa migodi na jinsi tunavyorudisha kwenye jamii,” alisema.
Kuhusu Rebuilding (Ujenzi Upya), Dk. Ngido alieleza kuwa migodi yote ilifanyiwa maboresho makubwa, ambapo ufanisi na uelewa wa kijiolojia uliongezwa, na maisha ya migodi hiyo kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi.
“Migodi yetu ambayo wakati Barrick inaichukua mwaka 2019 ilikuwa inategemewa kuisha 2026/2027, tumeongeza uhai wake hadi mwaka 2050. Bado tunaendelea na tafiti ili migodi iendelee kuleta manufaa kwa wananchi wetu,” alisema.
![]() |
| Baadhi ya washiriki na wadhamini wa Mkutano wa Tatu wa CEOs Forum 2025 wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko. |
Kwa upande wa Resilience (Ustahimilivu), alisema kampuni imewekeza zaidi kwenye teknolojia na usalama wa migodi, ikiwa ni pamoja na kutumia mashine za kisasa kama Taller Remote Machines.
“Tumewekeza zaidi kwenye teknolojia na tafiti. Migodi yetu sasa ina mashine za kisasa zinazosaidia katika usalama na kuongeza tija, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha migodi hii inafikia mwaka 2050,” alisema.
Dk. Ngido alieleza pia kuwa Barrick imewekeza zaidi ya trilioni 14 ndani ya nchi katika kipindi cha miaka minne iliyopita, huku zaidi ya asilimia 96 ya wafanyakazi wa migodi hiyo wakiwa ni Watanzania, na asilimia 47 wakitoka katika maeneo yanayozunguka migodi.
“Katika kipindi cha miaka minne, tumewekeza ndani ya nchi zaidi ya trilioni 14. Tumeajiri Watanzania kwa zaidi ya asilimia 96 na asilimia 47 kati yao wanatoka kwenye maeneo yanayozunguka migodi,” alisema.
Aliongeza kuwa Barrick imelipa zaidi ya trilioni 4 kama kodi na michango mingine kwa serikali, na kwamba kampuni hiyo inatoa dola 6 kwa kila wakia ya dhahabu inayouzwa, ambazo huwekezwa kwenye miradi ya kijamii kama afya na elimu kupitia Corporate Social Responsibility (CSR).
“Tunalipa kodi na michango mingine serikalini inayozidi trilioni nne. Hii inaonyesha kuwa tukizifuata 4R za Rais Samia vizuri, tunaweza kuleta matokeo chanya na kusapoti dira ya maendeleo ya Taifa,” alisisitiza Dk. Ngido.
Akihitimisha, alisema kuwa sababu kubwa ya Barrick kudhamini mkutano huo ni kutokana na imani ya kampuni kwa falsafa ya 4R, na kwamba mabadiliko yaliyopatikana ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali.
“Hayo ni machache ambayo tumeona tuyaseme sisi kama wadhamini wakubwa. Sababu
kubwa ya kuvutiwa kuja kusapoti ofisi ya Msajili wa Hazina ni kwa sababu tumeona tukifocus kwenye 4R tutaleta mabadiliko,” alisema.
Awali Kampuni hiyo ya Barrick yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga imetunukiwa cheti cha tuzo kwa kudhamini kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichomalizika leo jijini Arusha.





0 Comments:
Post a Comment