Waziri Mkuu Apongeza Ukuaji wa Thamani ya Soko la Hisa la Dar es Salaam Kufikia Trilioni 21


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepongeza Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa mafanikio makubwa katika kuongezeka kwa thamani ya soko hilo, ambayo imefikia shilingi trilioni 21 kufikia Julai 2025, pamoja na ongezeko la zaidi ya asilimia 246 kwenye mauzo ya hisa.



Ametoa pongezi hizo leo Jumanne, Agosti 26, 2025, alipotembelea ofisi za DSE zilizopo Morocco, jijini Dar es Salaam, ambapo pia ametangaza kununua hisa zenye thamani ya shilingi milioni 100 kama ishara ya kuunga mkono maendeleo ya sekta ya mitaji nchini.



"Hiki ni kielelezo cha ubunifu na mchango wa DSE katika kuendeleza uchumi jumuishi na endelevu wa Taifa letu. Hii hatuwezi acha ikapita, ni lazima tuwapongeze," amesema Majaliwa.

Amesema mafanikio hayo pia yanaonekana kwenye ongezeko la idadi ya wawekezaji hadi zaidi ya akaunti 683,000, pamoja na mauzo ya hatifungani yaliyofikia zaidi ya shilingi trilioni 3, zikiwemo hatifungani zenye maudhui ya kusaidia mazingira na jamii.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kuwekeza kupitia DSE kwa njia ya kidijitali:

"Watanzania wekeni kipaumbele cha kufanya uwekezaji kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa njia ya kidigitali ili kupata fursa ya kumiliki makampuni, kupata faida na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa letu."

Pia ameielekeza Wizara ya Fedha kuendelea kushirikiana na DSE katika kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na soko hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amesema Serikali imejipanga kukuza masoko ya mitaji kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Serikali imeweka mpango wa kuendeleza bidhaa mpya za kifedha kama hati fungani, kuimarisha mifumo ya kidijitali na kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje, ili kukuza soko la DSE," amesema Mwandumbya.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Charles Shirima, amesema matumizi ya teknolojia yamewezesha wananchi wengi zaidi, mijini na vijijini, kushiriki katika uwekezaji wa masoko ya mitaji.

"Kwa mfano, asilimia 24.33 ya mauzo ya hisa kwa mwaka 2024 yalifanyika kwa kutumia mifumo ya teknolojia ya habari, yakiwa yameongezeka kutoka asilimia 4.84 mwaka 2023," amesema Shirima, akitaja mifumo kama Sim Invest, Hisa Kiganjani, WekezaWHI na M-Wekeza.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Situmbeko, amesema soko hilo limeendelea kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

"Thamani ya mauzo ya hisa ilifikia shilingi bilioni 369.4 sawa na ongezeko la asilimia 246. Idadi ya hisa zilizouzwa ilikuwa milioni 272, ongezeko la asilimia 108. Hatifungani za Serikali na makampuni binafsi zilifikia jumla ya mauzo ya zaidi ya shilingi trilioni 3, kutoka trilioni 1.9 mwaka uliopita," amesema Situmbeko.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na watendaji wa DSE na kuhimiza kuendelezwa kwa ubunifu na uwazi katika kusimamia rasilimali za wawekezaji.

0 Comments:

Post a Comment