Serikali yataka Mashirika ya Umma kuiga Sekta Binafsi kuongeza ufanisi



Serikali imeyataka mashirika ya umma nchini kuiga mbinu za sekta binafsi ili kuongeza ufanisi, kupunguza utegemezi kwa Serikali na kuchangia zaidi katika uchumi wa Taifa.



Akihitimisha kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma Agosti 26, 2025 jijini Arusha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, alisema sekta binafsi zinafikiri vizuri na zinaweza kulipa mishahara na kodi bila kutegemea ruzuku, tofauti na baadhi ya mashirika ya umma ambayo bado yanaomba fedha za kujiendesha.



“Wakuu wa Taasisi za Umma mnapaswa kuziba mianya ya upotevu wa mapato. Fanyeni kazi ya kusimamia mashirika yenu ili mkawe mafundi wa kurekebisha taasisi zenu na kufikiri tofauti huku mkizingatia ubunifu kama zilivyo sekta binafsi,” alisema Biteko.



Aidha, alisisitiza mshirikiano baina ya wenyeviti na wakurugenzi wakuu, akisema hataki kusikia migongano baina yao. Pia aliwakumbusha kudumisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa amani ndiyo msingi wa ufanisi wa mashirika ya umma.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, alisema mashirika ya umma yana jukumu kubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 yenye lengo la kulifikisha Taifa katika uchumi wa kati wa juu, huku pato la Taifa likitarajiwa kufikia dola trilioni moja kutoka dola bilioni 85 za sasa.



“Hii sio kazi ndogo, lakini naamini tukiimarisha mashirika yetu ya umma, tutaweza kufikia azma hiyo. Lengo ni kuhakikisha mashirika haya yanachangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa na utekelezaji wa Dira 2050,” alisema Nyongo.



Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema mageuzi ya mashirika ya umma yameanza kuzaa matunda ambapo mashirika makubwa kama STAMICO, TANESCO na TPDC yameondokana na utegemezi wa ruzuku ya Serikali katika kuendesha na kulipa mishahara.

“Kujitoa katika utegemezi kunawezesha fedha za Serikali kuelekezwa kwenye miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Mchechu.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salim Kali, alisema Mkoa wa Arusha ni salama na unapokea wawekezaji wengi huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi trilioni tatu kwa miradi ya maendeleo ndani ya miaka minne.

Mkutano huo wa siku tatu uliowakutanisha wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi za umma ulikuwa na kaulimbiu: Kujenga Ushirikiano Endelevu katika Mazingira ya Ushindani wa Kimataifa, Wajibu wa Mashirika ya Umma.

0 Comments:

Post a Comment