Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yanaendelea vizuri, na akaongeza kuwa anaamini kundi la Hamas lipo tayari kumaliza mzozo huo wa miezi 21.
Trump alitoa kauli hiyo wakati alipomkaribisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya White House mjini Washington DC.
Trump, ambaye amekuwa akihusika moja kwa moja katika juhudi za kidiplomasia za kuleta utulivu katika eneo hilo, alisema kuwa Hamas “wanataka kukutana na wanataka kuwa na usitishaji huo wa mapigano.”
Kauli hiyo ya ghafla kwa waandishi wa habari ilikuja wakati ambapo duru za hivi punde za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas, yaliyofanyika nchini Qatar, yalimalizika bila mafanikio, ingawa yalitarajiwa kuendelea ndani ya wiki hiyo hiyo.
Akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu ni nini kinazuia makubaliano ya amani huko Gaza, Trump alisema kwa matumaini: “Sidhani kama kuna kizuizi.
Nadhani mambo yanakwenda vizuri sana.” Kauli yake ilionekana kuashiria matumaini makubwa kuhusu suluhu ya mzozo huo, ambao umesababisha maelfu ya vifo, uharibifu mkubwa, na mateso ya muda mrefu kwa raia wa Kipalestina.
Katika mkutano huo, Netanyahu naye alizungumzia suala la baadaye ya Wapalestina. Alisema kuwa Israel inafanya kazi kwa karibu na Marekani kutafuta nchi ambazo zitaweza kuwapa Wapalestina “maisha bora ya baadaye.” Alieleza kwamba: “Ikiwa watu wanataka kubaki, wanaweza kubaki, lakini kama wanataka kuondoka, wanapaswa kuondoka.”
Kauli hiyo imezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jumuiya ya kimataifa, kwani inaweza kufasiriwa kama ishara ya kuwahamisha Wapalestina kwa lazima kutoka Gaza – jambo ambalo linaweza kukiuka sheria za kimataifa.
Ofisi ya rais wa Palestina tayari imetoa msimamo wake, ikikataa vikali mipango yoyote ya kuhamisha Wapalestina, ikisisitiza kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa. Wameitaka jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa haki na heshima ya watu wa Palestina inalindwa.
Netanyahu pia alieleza kuwa Israel haitakubali kuondoa udhibiti wa usalama katika Ukanda wa Gaza, hata kama kutafikiwa makubaliano ya usitishaji mapigano.
Kwa maneno yake, alisema: “Israel daima itaweka udhibiti wa usalama.” Kauli hiyo inaonyesha kuwa pamoja na juhudi za amani, bado kuna msimamo mkali wa Israel kuhusu usalama na mamlaka katika Gaza.
Kwa upande mwingine, Hamas imepokea pendekezo la kusitisha mapigano kwa “mhemko chanya,” lakini haijathibitisha wazi kuwa italikubali. Mazungumzo yanayoendelea yanahusisha pia pendekezo la usitishaji wa mapigano wa siku 60, unaodhaminiwa na Marekani kwa ushirikiano na Qatar na Misri.
Pendekezo hilo linajumuisha hatua za kubadilishana mateka, kupeleka misaada ya kibinadamu, na kupanga mazungumzo ya muda mrefu kuhusu suluhisho la kudumu.
Mpango huo wa siku 60 unatarajiwa kuwa hatua ya kwanza kuelekea amani ya kudumu, lakini unakabiliwa na changamoto kutoka kwa makundi ya kisiasa ndani ya Israel na Hamas, pamoja na shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa inayotaka kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti.
Kwa sasa, dunia inatazama kwa karibu maendeleo ya mazungumzo haya, ambayo huenda yakaleta mwelekeo mpya katika historia ya mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina. Trump, ambaye amekuwa akijipambanua kama mwepesi wa kupatanisha migogoro ya kimataifa, anaonekana kuwekeza matumaini makubwa katika mafanikio ya mpango huu wa amani. Hata hivyo, iwapo kweli utazaa matunda, bado ni suala linalosubiriwa kwa tahadhari na matumaini.

0 Comments:
Post a Comment