TAWA Yafungua Milango kwa Wawekezaji Kwenye Sekta ya Utalii



Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetangaza rasmi kuwa milango ya uwekezaji bado iko wazi, huku ikisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya maliasili na utalii.





Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, amesema taasisi hiyo inakaribisha wawekezaji wote kushiriki katika fursa mbalimbali zilizopo ndani ya maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

"TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji, unapotaka kuwekeza unakaribishwa sana," amesema Maganja. Ameongeza kuwa mazingira yaliyowekwa na serikali yanalenga kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kwa nia ya kukuza sekta ya utalii nchini.

"Fursa hizi zinakuwa wazi kwa wawekezaji wote na ndio maana tuko hapa kuwatangazia waje kuwekeza katika hii taasisi," ameongeza Maganja.

Kwa mujibu wa Maganja, maeneo mbalimbali yanaendelea kufunguliwa kwa uwekezaji, yakiwemo Makuyuni Wildlife Park (Arusha), Wami-Mbiki (Morogoro), Mpanga/Kipengere (Mbeya na Njombe), Tabora ZOO, Ruhila ZOO na maeneo mengine yenye vivutio vya kipekee.

Amesisitiza kuwa maeneo hayo yana rasilimali adimu na mandhari ya kuvutia ambayo yanatoa fursa kubwa kwa uwekezaji endelevu, huku yakihifadhi na kulinda maliasili za taifa.



Kwa upande wake, Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka TAWA, Gladson Mlay, amewataka wananchi kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo ili kujionea vivutio vilivyopo.

“Tunawaalika wananchi waje waone wanyamapori hai kama simba, chui, fisi, mamba na spishi mbalimbali za ndege,” amesema Dkt. Mlay.

Ameongeza kuwa maonesho hayo pia ni fursa kwa wananchi kuonja kitoweo cha nyamapori choma kilichoandaliwa kwa ubunifu na umahiri wa hali ya juu.

“Kwa wale ambao wanasema hawajawahi kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa, mishikaki pia ipo na nyama ya kupeleka nyumbani. Kwahiyo watu wote mnakaribishwa mje kuonja, kula na kuona kama kweli maliasili ni za kwetu wote,” amesema Dkt. Mlay.

TAWA imeendelea kusisitiza dhamira ya kuhakikisha kuwa rasilimali za maliasili zinatumika kwa njia endelevu, huku ikitoa fursa za kiuchumi kwa Watanzania na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani.

0 Comments:

Post a Comment