Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezindua rasmi zoezi la chanjo ya mifugo katika Kijiji cha Mokilal, Tarafa ya Ngorongoro, Mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa miaka mitano (2025–2030) wa utoaji wa chanjo kwa mifugo kote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kuboresha afya ya mifugo, kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mifugo na kuinua kipato cha wafugaji.
“Mpango huu wa kitaifa wa chanjo ya mifugo ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 16 Juni 2025, Bariadi mkoani Simiyu.
Serikali imetenga shilingi bilioni 216 kwa utekelezaji wa mpango huu na mpaka sasa zaidi ya bilioni 62 zimeshatolewa kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema Dkt. Kijaji.
Katika kuhakikisha wafugaji wananufaika moja kwa moja, Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali imepunguza bei ya kuchanja mifugo ambapo Ng’ombe mmoja atachanjwa kwa shilingi 500 badala ya 1,000 na Mbuzi au Kondoo kwa shilingi 300 badala ya 500.
“Tunataka kila mfugaji aweze kushiriki. Hii ni juhudi ya Serikali kuhakikisha wafugaji wanapata huduma hii kwa gharama nafuu,” alisisitiza Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benezeth Lutege, alieleza kuwa chanjo ya mifugo inalenga kuongeza thamani ya mifugo katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kurahisisha upangaji wa maeneo ya malisho.
“Kupitia zoezi hili tutapata idadi kamili ya mifugo na wamiliki wao, na taarifa hizi zitawekwa katika mfumo wa kielektroniki kupitia barcode za hereni za utambuzi kwa kila mnyama. Hii itasaidia pia wafugaji kutumia taarifa hizi kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha,” alisema Lutege.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, alieleza kufurahishwa na muitikio mkubwa wa wananchi wa Ngorongoro na maeneo mengine ya mkoa huo katika kushiriki zoezi la chanjo.
“Wananchi wameonesha ushirikiano mkubwa. Tutaendelea kuhamasisha wafugaji wote kuchanja mifugo yao ili kutimiza azma ya Rais ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta ya mifugo,” alisema Kihongosi.
Naye Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, aliishukuru Serikali kwa kuliangalia kwa jicho la huruma eneo la Ngorongoro na kuwapatia chanjo muhimu kwa mifugo yao.
“Tunawashukuru kwa kusikiliza kilio cha wafugaji. Nawaomba wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hili, kwa kuwa litatusaidia kuondokana na magonjwa ya mifugo na kuboresha afya pamoja na thamani ya mifugo yetu,” alisema Shangai.
Zoezi la chanjo ya mifugo linatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya ufugaji nchini kwa kuhakikisha mifugo inakuwa na afya bora, yenye tija kiuchumi na kuchangia pato la taifa kwa kiwango kikubwa.







0 Comments:
Post a Comment