Mchujo CCM Kuanzia Julai 4, Mapato ya Fomu Yagusa Mabilioni

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa uchujaji wa majina ya wanachama waliowasilisha fomu za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi za Ubunge, Udiwani na Uwakilishi, ambapo jumla ya watia nia zaidi ya 20,000 wamejitokeza. 


Kupitia mchakato huo, chama kimekusanya mapato ya mabilioni ya shilingi kutokana na mauzo ya fomu, fedha ambazo zitaelekezwa katika kuimarisha shughuli za kisiasa na maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.



Akizungumza Julai 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema mchakato wa uchujaji utaanza kesho Julai 4, 2025 katika ngazi ya kata na kuendelea hadi Julai 19, 2025.

“Vikao vya uchujaji vinaanza kwa maana tarehe 4, 2025, katika kata zetu wataanza kukaa kamati za siasa kutoa mapendekezo kwa ajili ya wagombea hawa kwa ajili ya uteuzi wa madiwani walioomba katika kata, viti maalum,” alisema Makalla.

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, Kamati za Siasa za mikoa zinatarajiwa kufanya vikao vyake Julai 9, 2025 kwa ajili ya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi za udiwani.

“Kamati za siasa za mkoa kwa ratiba ya chama zinatarajia kukaa Julai 9, 2025, kufanya uteuzi kwa nafasi wanaoomba udiwani,” aliongeza Makalla.

Kwa upande wa nafasi za ubunge na uwakilishi, uteuzi wa mwisho utafanywa na Kamati Kuu ya CCM, ambapo wagombea watatu kutoka kila jimbo watapendekezwa.

“Kwa mujibu wa ratiba yetu, inaonesha ni Julai 19, 2025, itafanya uteuzi wa mwisho kwa maana wagombea wale watatu watatu,” alisema Makalla.

Takwimu zilizotolewa zinaonesha kuwa jumla ya wanachama 4,109 wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea ubunge katika majimbo 272 ya uchaguzi. Kati ya hao, 3,585 wanatoka Tanzania Bara na 524 Zanzibar.

Kwa upande wa nafasi za uwakilishi visiwani Zanzibar, wanachama 503 wamechukua fomu. Kwa upande wa Jumuiya ya Wanawake (UWT), waliochukua fomu ni 623, kati yao 91 ni wa makundi maalumu kutoka bara na wanane kutoka Zanzibar. Pia, Viti Maalum uwakilishi Zanzibar ni tisa.

Kwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wanachama 161 wamechukua fomu, wakiwemo 154 kutoka bara na saba kutoka Zanzibar. Jumuiya ya Wazazi nao wamewakilishwa na wanachama 62; 55 kutoka bara na saba kutoka Zanzibar.

Kwa ujumla, waliochukua fomu za kuwania ubunge na uwakilishi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni 5,474.

Makalla alisema katika Kata 3,960, zaidi ya wanachama 15,000 wamechukua fomu za kuwania nafasi za udiwani, hali inayodhihirisha mwitikio mkubwa wa wanachama kushiriki katika nafasi za uongozi kupitia CCM.

Mchakato huu wa ndani ya chama ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ambapo CCM inaendelea kujiimarisha kwa kuhakikisha inapata wagombea bora watakaoiwakilisha vyema chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi.

0 Comments:

Post a Comment