Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa, ametangaza rasmi kutogombea tena ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na kuwataka wana-Ruangwa kuendeleza mshikamano na maendeleo aliyoanzisha kwa kipindi cha miaka 15 ya utumishi wake.
Majaliwa ametangaza uamuzi huo leo, Julai 2, 2025, wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
“Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili kaulimbiu yetu ya ‘Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana’ iweze kusonga mbele zaidi,” amesema Majaliwa.
Aidha, ametoa shukrani kwa wananchi wa Ruangwa kwa kumuunga mkono tangu achaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010.
“Nawashukuru sana kwa ushirikiano mlionipa kwa miaka yote.
Nimetumikia kwa moyo mmoja, sasa ni wakati wa wengine kuendeleza kule tulikoishia,” amesema.
Majaliwa pia ametoa wito kwa wana-Ruangwa kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea atakayesimamishwa na CCM pamoja na viongozi wakuu wa chama hicho.
“Viongozi wetu Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dk. Nchimbi watakapokuja tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga kura tuwapigie kura nyingi za kutosha,” amesisitiza.
Kwa upande mwingine, makada watano wa CCM wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ruangwa, Abbas Mkweta, amesema hadi kufikia leo majira ya saa kumi jioni, ni makada watano waliokuwa wamechukua na kurejesha fomu, huku akibainisha kuwa dirisha la uchukuaji fomu lilifunguliwa Juni 26.
“Wanachama hao ni Bakari Nampenya, Philip Makota, Fikiri Liganga, Hashim Mparuka na Kaspa Muya. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kupumzika na kuwaachia wengine,” amesema Mkweta.
Hashim Mparuka, mmoja wa waliochukua fomu, amesema anajitokeza kuendeleza kazi kubwa iliyofanywa na Majaliwa:
“Nina heshima kubwa kwa kazi ya Mheshimiwa Majaliwa, na sasa najitokeza kuchukua mikoba ili kuendeleza maendeleo ya Ruangwa,” amesema Mparuka.
Awali, Juni 26, wakati akihitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma, Majaliwa aliwashukuru wananchi wa Ruangwa na kusema atarejea tena kuwania ubunge.
Hata hivyo, Uamuzi huo wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Ruangwa unaacha maswali mengi kwa wachambuzi wa siasa na wananchi kwa ujumla.
Zikiwa zimepita siku chache tu tangu atangaze bungeni kuwa atarejea kuwania ubunge, hatua yake ya ghafla ya kubadili msimamo inazua sintofahamu juu ya sababu halisi za mabadiliko hayo.
Wengi wanajiuliza kama ni uamuzi wa hiari wa kisiasa, ishara ya maandalizi ya mabadiliko makubwa ndani ya serikali, au kama kuna sababu nyingine zilizomlazimu kujiondoa.
Hadi sasa, Majaliwa hajatoa maelezo ya kina kuhusu kile kilichomsukuma kuachia nafasi hiyo ambayo ameishikilia kwa miaka 15..
Kwa uamuzi huu, historia mpya inaanza kuandikwa katika siasa za Ruangwa, huku wananchi wakisubiri kwa hamu kuona nani atakayechaguliwa kuendeleza dira ya maendeleo ya jimbo hilo.



0 Comments:
Post a Comment