Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma yameibuka kuwa zaidi ya tukio la kikazi, baada ya banda la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuvutia idadi kubwa ya wananchi waliotaka kufahamu kwa undani vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo maarufu duniani.
Kutoka kwa wananchi wa Dodoma hadi wageni kutoka mikoa ya jirani, wengi walionekana kuvutiwa na elimu waliyoipata kuhusu maeneo ya kipekee kama Bonde la Kreta ya Ngorongoro, nyayo za Laitole, Bonde la Olduvai Gorge, Kreta ya Empakai, pamoja na mchanga unaohama – vivutio ambavyo vimeifanya Ngorongoro kuwa lulu ya utalii wa Tanzania.
Akizungumza na wananchi waliotembelea banda hilo, Afisa Utalii kutoka Idara ya Huduma za Utalii na Masoko, Joseph Mzaga alisema:
“Tumepokea wageni mbalimbali walioweza kufika kwenye banda letu ambao wengi wao walitamani kufahamu zaidi kuhusiana na vivutio vya utalii, namna ya kufika hifadhini, viingilio na taarifa zingine muhimu za kuwasaidia kwa ajili ya maandalizi ya safari zao.”
Naye Agatha Antony, mkazi wa Dodoma, hakuficha furaha yake baada ya kupata taarifa alizohitaji kuhusu safari yao inayokuja ya kutembelea hifadhi hiyo:
“Mimi pamoja na wafanyakazi wenzangu kutoka taasisi ya Pharma Afrika tunajiandaa na safari ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro na leo nimefurahi zaidi kwani nimeweza kufika hapa na nimepata taarifa ambazo zitatusaidia kwenye maandalizi yetu mfano viingilio, usafiri na vivutio ambavyo tutaweza kuvitembelea.”
Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23, ikiwa ni jukwaa la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa. Mwaka huu, maadhimisho haya yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Himiza Matumizi ya Mfumo wa Kidijitali Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.”
Kwa upande wa NCAA, ushiriki wao katika maonesho haya ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza utalii wa ndani na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo katika hifadhi hiyo adimu, inayotajwa kuwa moja ya maajabu ya dunia kwa urithi wake wa kipekee wa asili na historia.




0 Comments:
Post a Comment