Putin: Niko Tayari Kukutana na Zelensky



Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema kuwa yuko tayari kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, lakini kikao hicho kitawezekana tu katika hatua ya mwisho ya mazungumzo ya amani ambayo yanalenga kumaliza vita vinavyoendelea kwa mwaka wa nne sasa kati ya nchi hizo mbili jirani.

Katika hotuba yake alipokuwa mjini Kremlin baada ya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Toh Lam, Putin alisema:

“Mazungumzo yanaweza kufanikishwa iwapo kutakuwa na dhamira ya kweli kutoka pande zote. Niko tayari kukutana na Zelensky, lakini ni katika awamu ya mwisho ya mazungumzo ya amani.”

Hata hivyo, alisisitiza masharti makali ambayo ni pamoja na Ukraine kukubali kupoteza maeneo zaidi, kuachana na ushirikiano wa kijeshi na mataifa ya Magharibi na kutambua mamlaka ya Urusi katika maeneo yenye mzozo mashariki mwa Ukraine.

“Lazima kuwe na mkataba wa amani ambao unahakikisha uthabiti wa muda mrefu na kuzuia migogoro ya baadaye,” aliongeza.

Masharti hayo yamepingwa vikali na viongozi wa Ukraine. Kwa mujibu wa maafisa wa Kyiv, Urusi inatumia mazungumzo hayo kama mbinu ya kupunguza shinikizo la kimataifa huku ikiendeleza mashambulizi ya kijeshi.

Katika hatua nyingine, Putin alitoa onyo kali kwa Ujerumani kuhusu mipango yake ya kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ya Taurus.

“Utoaji wa makombora ya Taurus kwa Ukraine utamaanisha Ujerumani inahusika moja kwa moja kwenye vita,” alionya Putin.

Licha ya mvutano huo, alisema yuko tayari kuzungumza na Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, lakini alitilia shaka nafasi ya Berlin kuwa mpatanishi huru.

“Ujerumani haiwezi tena kuaminika kuwa mpatanishi baada ya msimamo wake wa wazi wa kijeshi kwa Ukraine,” alisema.

Putin pia aliongeza mashaka kuhusu uhalali wa mamlaka ya Rais Zelensky chini ya sheria ya kijeshi, akihoji ikiwa ana mamlaka kamili ya kufanya maamuzi ya kitaifa.

Wakati huo huo, Ukraine imekumbwa na shambulio la nguvu lililofanywa na Urusi dhidi ya jengo la makazi katika wilaya ya Solomianskyi mjini Kyiv. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 28 na kuacha wengine wengi wakiwa majeruhi au kupotea.

Kwa mujibu wa mamlaka ya Ukraine, makombora 32 na droni zaidi ya 440 zilitumika katika shambulio hilo lililotajwa kuwa baya zaidi mwaka huu.
Waokoaji walitumia kreni na mbwa waliopokea mafunzo maalum kujaribu kuokoa manusura kutoka kwenye kifusi.

“Usiku ule ulikuwa wa hofu. Tulijificha kwenye korido kwa saa nyingi tukiwa tumesikia milio ya milipuko karibu kabisa,” alisema mmoja wa manusura.

Katika taarifa kutoka ubalozi wa Marekani mjini Kyiv, Marekani ililaani vikali shambulio hilo.

“Shambulio hili ni kinyume na wito wa Rais Trump wa kusitisha mauaji na kumaliza vita,” ilisema taarifa hiyo.

Rais wa Marekani, Donald Trump, katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Canada alisema:

“Nitakutana na Putin haraka sana. Dunia inahitaji suluhu ya amani kwa mzozo huu wa Ukraine.”

Hata hivyo, Ukraine imeikosoa jumuiya ya kimataifa kwa “kupoteza mwelekeo” na kushindwa kutoa msukumo wa kutosha kwa mchakato wa amani, ikilaumu mvuto wa mizozo mingine kama ile ya Mashariki ya Kati na vita vya kibiashara vya kimataifa.

“Ukraine imeachwa iendelee kupigana vita vya kujitetea huku dunia ikiwa imesongeshwa na masuala mengine,” alisema mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje ya Ukraine, bila kutajwa jina.

Kwa sasa, matumaini ya kumalizika kwa vita hayo bado yapo katika hali ya mashaka, huku pande zote zikiendelea kushikilia misimamo mikali na maelfu ya raia wakiendelea kupoteza maisha na makazi.

0 Comments:

Post a Comment