Mkuu wa Jeshi la Iran Ali Shadmani Auuawa Katika Makabiliano na Israel; Kiongozi Mkuu Khamenei Asema Iran Haitasita Kujibu Mashambulizi

 


Ali Shadmani, mkuu wa kituo cha utoaji amri cha makao makuu ya kijeshi ya Khatam al-Anbia ya Iran, amefariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa makabiliano ya kijeshi na Israel, limeripoti Shirika la Habari la Fars. Jeshi la Israel lilitangaza tarehe 17 Juni kuwa limemuua Shadmani, akitambuliwa kama "mkuu wa majeshi wa Iran na kamanda wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi wa nchi hiyo."

Shadmani alikuwa mrithi wa Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, aliyewahi kuwa mkuu wa kituo cha amri cha makao makuu ya IRGC ya Khatam al-Anbia, ambaye naye aliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel mnamo Juni 13, usiku wa kwanza wa makabiliano ya kijeshi kati ya Israel na Iran.

Makao Makuu ya Kati ya Khatam al-Anbia yanahusika na uratibu kati ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na vikosi vya kawaida vya kijeshi, na hutumika kama kamandi kuu wakati wa vita chini ya mamlaka ya moja kwa moja ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.



Katika muktadha huu, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametoa onyo kali akisema kuwa Iran haitasita kujibu mashambulizi yoyote dhidi yake, hasa yale yanayolenga vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyopo katika eneo la Mashariki ya Kati. Khamenei aliongeza kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu yatakuwa na "gharama kubwa."

Katika hotuba yake ya kwanza ya televisheni tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Israel, Khamenei alisema:

"Iran tayari ililenga kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani Mashariki ya kati, iliyoko Qatar, baada ya Marekani kujiunga na mashambulizi ya Israel. Kwa kuzingatia uwezo wetu wa kufikia maeneo muhimu ya Marekani katika Mashariki ya Kati na kuchukua hatua dhidi yao wakati wowote inapohisi sio jambo dogo."

Kiongozi huyo pia alijibu kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alisema Iran lazima ijisalimishe, kwa kusema:

"Hili halihusiani tena na urutubishaji wa urani au sekta ya nyuklia pekee — ni juu ya kulazimisha Iran kunyenyekea. Bila shaka, kauli kama hiyo ni kujitutumua mno kutoka katika kinywa cha rais wa Marekani."

Katika upande mwingine, Rais Trump alithibitisha kuwa Marekani ingeweza kushambulia Iran tena ikiwa taifa hilo lingerejea kwenye mpango wa kurutubisha madini ya urani.



Aidha, Bunge la Iran limepitisha mswada wa kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa sababu ya kushindwa kwa IAEA kulaani mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Iran na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran. Msemaji wa Baraza la Katiba la Iran, Tahan Nazif, amesema mswada huo utawasilishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian kwa idhini ya mwisho, na utaruhusu Iran kufaidika na haki zote chini ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), hasa kuhusu urutubishaji wa urani.

Wakati huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amepinga hatua hiyo ya Iran, akitaja nchi hiyo kama mshirika mkuu wa Moscow.

Mazishi ya kiserikali kwa makamanda wakuu wa kijeshi wa Iran, akiwemo Ali Shadmani, pamoja na wanasayansi wakuu waliouawa katika mfululizo wa mashambulizi haya, yatafanyika siku ya Alhamisi na Jumamosi.


0 Comments:

Post a Comment