URUSI YAAHIDI KUISAIDIA IRAN KATIKA MGOGORO NA ISRAEL NA MAREKANI




Moscow, Juni 23, 2025 – Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameikosoa vikali Marekani na Israel kufuatia mashambulio yao dhidi ya Iran, akiyaita “uchokozi usio na sababu.” Katika mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, uliofanyika leo mjini Moscow, Putin ameahidi kuwa Urusi iko tayari kuisaidia Iran katika kukabiliana na hali inayoendelea Mashariki ya Kati.


Putin amesema Urusi haioni uhalali wowote wa hatua zilizochukuliwa na Marekani, akiashiria kuwa njia pekee ya kurejesha utulivu ni kupitia mazungumzo na ushirikiano wa kidiplomasia, sio mashambulio ya kijeshi.


Abbas Araghchi amepongeza msimamo wa Urusi, akisema kuwa “sauti ya haki” ina nguvu katika wakati huu ambapo Iran inashambuliwa na kile alichokiita ni "muungano wa mashambulizi ya kipropaganda na kijeshi".


Mashambulio ya Kisasi Yazidi Kuongezeka


Hali ya taharuki Mashariki ya Kati inaendelea kuongezeka kwa kasi. Leo hii, Israel imefanya mashambulio makubwa dhidi ya Tehran, yakilenga majengo ya serikali, barabara zinazoelekea kwenye kituo cha nyuklia cha Fordo, pamoja na gereza la Evin – jela linalojulikana kwa kuwahifadhi wafungwa wa kisiasa.


Haya yamekuja baada ya Iran kuishambulia Israel kwa makombora na droni, ikiwa ni majibu kwa shambulio kubwa lililofanywa na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, ikiwemo Fordo na Natanz. Marekani ilitumia ndege za kivita na mabomu ya ardhini kupenya miamba ya milima iliyojenga ngome za nyuklia za Iran.


Iran imeapa kulipiza kisasi kwa mashambulio hayo, na tayari imeshambulia maeneo kadhaa ndani ya Israel na kambi ya kijeshi ya Marekani iliyopo Qatar. Hadi sasa, Marekani haijathibitisha kuwepo kwa majeruhi lakini imetoa tahadhari kali kwa raia wake walioko Mashariki ya Kati kutafuta maeneo salama ya kujihifadhi.


Kauli Tofauti kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa


Wakati Urusi ikisimama upande wa Iran, mataifa mengine makubwa yamechukua misimamo tofauti. Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amesema hana sababu ya kukosoa hatua za Israel na Marekani, akieleza kuwa “kuacha hali iendelee kama ilivyokuwa pia haikuwa chaguo.”


Hali hii imezua mgawanyiko mkubwa ndani ya jumuiya ya kimataifa, ambapo baadhi ya mataifa kama China na Italia wameitaka Iran kujizuia kuchukua hatua za kiuchumi kama kufunga Mlango Bahari wa Hormuz – njia muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani.


Mazungumzo ya dharura yanaendelea kufanyika katika miji mbalimbali ya dunia, likiwemo Brussels, ambako mawaziri wa mambo ya nje wanajadili njia za kupunguza mivutano kabla ya hali kugeuka kuwa vita kamili ya kikanda.


Hofu ya Vita Kuu Mashariki ya Kati


Mashirika ya ndege ya kimataifa yameanza kufuta au kupunguza safari kuelekea Mashariki ya Kati kutokana na hatari za angani. Huku hayo yakiendelea, Iran inaonekana kuwa haiko tayari kurudi nyuma, hasa baada ya kuungwa mkono na Urusi.


Hofu sasa imejikita kwenye uwezekano wa kuporomoka kwa utawala wa Iran, jambo linalotajwa na baadhi ya wachambuzi kuwa linaweza kuibua mabadiliko makubwa ya kisiasa katika eneo hilo. Wairani walioko uhamishoni, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu, wanasema mabadiliko hayo ni lazima yawe ya ndani, si ya kulazimishwa kutoka nje.


Wakati dunia inatazama kwa wasiwasi, pande zote zinatoa kauli kali, zikijiandaa kwa hatua zaidi. Juhudi za kidiplomasia zinaendelea, lakini hakuna dalili ya makubaliano ya karibu, huku risasi zikiendelea kupigwa, makombora kurushwa, na hofu ya vita kubwa kushamiri.


0 Comments:

Post a Comment