Katika kikao chake na Maafisa na Askari wa hifadhi hiyo, Kamishna Kuji alisisitiza kuwa kila mtumishi ana haki ya kujiendeleza kielimu, haki ya kupata matibabu bora, likizo, kupandishwa cheo pindi anapokidhi vigezo vya kiutumishi, pamoja na kuthaminiwa kwa kazi anayoifanya.
“Kila mtumishi ana haki husika, lakini pia Mwajiri ana matarajio ya kuona uwajibikaji madhubuti kutoka kwao,” alibainisha Kamishna Kuji.
Akimkaribisha Kamishna katika hifadhi hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kusini, Godwell Meng’ataki, alitoa pongezi kwa Serikali kwa juhudi zake katika kuboresha hifadhi na kukuza utalii, hasa katika ukanda wa Kusini.
“Tumeshuhudia idadi kubwa ya watalii. Kipekee shukrani zetu zimfikie Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake. Kupitia filamu maarufu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ na ‘Amazing Tanzania’, hifadhi za kusini zimeanza kuona matunda kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii na wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika maeneo haya,” alisema Meng’ataki.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi, Dkt. Emilian Kihwele, aliishukuru Bodi ya Wadhamini ya TANAPA pamoja na Menejimenti ya Shirika kwa namna wanavyowawezesha watendaji wa hifadhi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Kwa mwaka wa fedha ujao wa 2025/2026, Hifadhi ya Taifa Katavi imejipanga vilivyo katika kuhifadhi na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hii, sambamba na kukuza mapato yatokanayo na shughuli za utalii,” alisema Dkt. Kihwele.
Kwa upande wao, Maafisa na Askari Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Katavi walipongeza juhudi za Serikali na TANAPA kwa namna viongozi wake wanavyowatembelea, kuwasikiliza na kushirikiana nao kupanga mikakati ya kuimarisha taasisi.
“Nikupongeze Afande Kamishna Kuji. Licha ya majukumu uliyonayo unatoka na kuja kuzungumza na askari. Tumekuona ukitembelea hifadhi mbalimbali na sasa umefika hapa Katavi. Ukaribu huu unatia hamasa na kuongeza morali ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema Askari Uhifadhi Daraja la Kwanza, Erasto Majabe.
Serikali kupitia TANAPA inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii katika maeneo ya nyanda za juu Kusini ili kuwezesha watalii wengi zaidi kutembelea maeneo yaliyohifadhiwa katika ukanda huo, na kupunguza utegemezi wa hifadhi za kaskazini pekee.
Ziara ya Kamishna Kuji katika Hifadhi ya Taifa Katavi imetoa msukumo mpya wa ari, weledi, na mshikamano miongoni mwa Maafisa na Askari Uhifadhi katika kuendeleza dhamira ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa kwa uendelevu.





0 Comments:
Post a Comment