Waziri Mkuu wa Uholanzi, Dick Schoof, ametangaza kuwa nchi hiyo itafanya uchaguzi mpya kufuatia kusambaratika kwa serikali ya muungano, baada ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha PVV kujiondoa kutokana na mvutano kuhusu sera za uhamiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini The Hague, Waziri Mkuu Schoof alisema:
“Serikali yangu itaendelea kuongoza hadi uchaguzi mpya utakapofanyika.”
Hatua ya chama cha PVV kujiondoa imesababisha mgogoro wa kisiasa na kuleta hitaji la kurejea kwa wananchi kuwa na sauti kuhusu mustakabali wa taifa hilo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kundi la Upinzani Bungeni, Frans Timmermans, alisisitiza umuhimu wa kuwa na serikali inayojenga umoja na kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto za kitaifa.
“Nadhani ni fursa kwa vyama vyote vya kidemokrasia kujizuia na misimamo mikali, kwa sababu ni wazi ukiwa na misimamo mikali, huwezi kuongoza. Mambo yakiwa magumu, wanakimbia,” alisema Timmermans.
“Tunahitaji kuandaa uchaguzi. Kwa sababu watu wanahitaji kuwa na usemi tena. Tunahitaji hilo.”
Ingawa tarehe rasmi ya uchaguzi mpya bado haijatangazwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa uchaguzi huo utafanyika kabla ya majira ya mapukutiko.
Mgogoro huu wa kisiasa unakuja miezi michache tu baada ya Dick Schoof kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, hatua iliyofuata mazungumzo marefu ya kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi uliopita.
Uholanzi sasa inaingia katika kipindi cha mpito cha kisiasa, huku macho ya wananchi na jumuiya ya kimataifa yakiwa kwenye hatua zinazofuata kuelekea uchaguzi mpya.

0 Comments:
Post a Comment