Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, ameongoza Misa Takatifu ya shukrani kwa mara ya kwanza leo, Juni 3, 2025, katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Kurasini, jijini Dar es Salaam, baada ya kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa kwa karibu mwezi mmoja kufuatia tukio la kushambuliwa.
Ibada hiyo imehudhuriwa na mapadri, watawa pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti ya TEC, ikiwa ni ishara ya mshikamano na shukrani kwa Mungu kwa uponyaji wa Padri Kitima.
Akihubiri katika misa hiyo, Padri Kitima aliwashukuru wote waliomuombea na kumtumia salamu za pole wakati wa kipindi kigumu cha matibabu. Alieleza kuwa kurejea kwake ni ushuhuda wa wema wa Mungu na ushindi wa imani dhidi ya hofu.
“Tunamshukuru Mungu kwa wema wake. Pia tunawashukuru wote walioguswa na tukio lile. Tuombe Kanisa lizidi kuwa imara bila kutetereka. Kanisa Katoliki ni taasisi inayotegemewa na wengi, ni sauti ya wasio na sauti, ni msindikizaji wa wanyonge,” alisema kwa sauti ya matumaini.
Katika hotuba yake, Padri Kitima alihimiza kuwa Kanisa linapaswa kuendelea kuwa mwanga na tumaini kwa Watanzania licha ya changamoto mbalimbali, na kuwataka wafanyakazi wa TEC kuyatazama matukio yaliyopita kwa jicho la imani.
“Mungu hatakaa kimya; atajibu sala zetu. Tuwe imara katika kazi zetu. Tukumbuke kuwa hata mitume walipata misukosuko, lakini hawakurudi nyuma. Nasi tusirudi nyuma, tubaki thabiti katika imani,” aliongeza kwa msisitizo.
Ibada hiyo imeacha alama ya mshikamano, matumaini na imani miongoni mwa washiriki, huku wengi wakieleza kurejea kwa Padri Kitima kama ishara ya ujasiri na neema ya Mungu inayoshinda giza la hofu na vurugu.



0 Comments:
Post a Comment