Monduli, Tanzania – Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Isimani, mkoani Iringa, huku akimtaka Mbunge wa sasa, William Lukuvi, kutekeleza ahadi yake ya kutogombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Lumilo Hotel, Manispaa ya Iringa, Kiswaga alisema ameamua kujitosa kuwania ubunge kutokana na wito mkubwa kutoka kwa wananchi wa Isimani ambao, kwa mujibu wake, wanataka mabadiliko ya uongozi baada ya zaidi ya miongo mitatu ya utawala wa Lukuvi.
“Mimi sijatumwa na Rais kama wengine wanavyojinadi, bali ninakuja kwa nia ya dhati inayotokana na umoja wa wana-Isimani wanaotaka mwelekeo mpya wa maendeleo,” alisema Kiswaga.
Katika maelezo yake, DC Kiswaga alidai kuwa Lukuvi aliwahi kutamka hadharani na pia katika vikao vya ndani vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa hatagombea tena nafasi ya ubunge.
“Mwaka 2022 tulikutana maeneo ya Shoppers Plaza jijini Dodoma, ambapo Lukuvi alinieleza binafsi kuwa hatagombea tena. Kauli hiyo aliirudia mwaka 2020 wakati wa kampeni na pia kwenye vikao vya chama. Sasa ni wakati wa kutekeleza ahadi hiyo,” alisisitiza.
Kiswaga pia alieleza wasiwasi wake juu ya kile alichokiita "mazingira ya vitisho" dhidi ya wagombea na wananchi ndani ya jimbo hilo, hali aliyoitafsiri kama ishara ya kupotea kwa demokrasia ya kweli ndani ya chama na jamii kwa ujumla.
“Uongozi si urithi. Ni lazima tuamini katika kubadilishana vijiti. Nia yangu ni kuleta kasi mpya ya maendeleo ambayo wananchi wanaitaka na wanaihitaji sasa zaidi ya wakati mwingine wowote,” alisema.
William Lukuvi, ambaye amehudumu kama Mbunge wa Isimani tangu miaka ya 1990 na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, bado hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu kama atagombea au la katika uchaguzi ujao.
Kwa tangazo hili la Kiswaga, kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Isimani kinaonekana kuanza kwa joto la kisiasa, huku macho yakielekezwa kwa uamuzi wa Lukuvi – kama atatekeleza kauli yake ya kutogombea tena au atajitosa tena kwenye kinyang’anyiro hicho.

0 Comments:
Post a Comment