Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetambua mchango mkubwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mafanikio ya ushindi wa tuzo ya European Award for Quality Choice Achievement 2025 kutoka taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR) nchini Sweden.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya tuzo hiyo iliyofanyika Juni 2, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Kamishna wa Uhifadhi CPA (T) Musa Nassoro Kuji alisema:
"Shirika letu linaitoa tuzo hii kwa heshima ya mchango wa Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kupitia filamu za 'The Royal Tour' na 'Amazing Tanzania'. Hili ni jambo kubwa ambalo limelifanya taifa letu litambuliwe kwa upekee kimataifa."
Tuzo ya ESQR 2025 ni ya sita mfululizo kushindwa na TANAPA tangu mwaka 2020, ikiwa ni ishara ya uendelevu wa utoaji huduma bora katika sekta ya utalii na uhifadhi nchini.
Kauli mbiu ya "TANAPA Nyumbani kwa Tuzo" ilitawala hafla hiyo, ikiashiria fahari na mafanikio ya pamoja kwa shirika na taifa kwa ujumla.
Kupokelewa kwa tuzo hii kumeweka Tanzania katika ramani ya dunia kama nchi inayoongoza kwa huduma bora za utalii na uhifadhi, huku mchango wa uongozi wa juu wa taifa ukiendelea kuonekana kama sehemu muhimu ya mafanikio hayo.




0 Comments:
Post a Comment