WAZIRI MCHENGERWA AAGIZA MADIWANI WABAKI NA VISHIKWAMBI,

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametoa agizo rasmi kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba vishikwambi vilivyokuwa vikitumika na madiwani waliomaliza muda wao havirejeshwi, bali wabaki navyo kama sehemu ya vitendea kazi vyao binafsi.



Akizungumza kwa njia ya simu tarehe 20 Juni 2025 kupitia simu ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, Waziri Mchengerwa alisema:

“Vifaa hivi walivyokuwa wakitumia ni vya kwao wenyewe. Madiwani waendelee kubaki navyo kwa sababu ndani yake kuna taarifa binafsi, barua pepe, mawasiliano ya familia zao na kazi walizozifanya kwa kipindi chao cha uongozi.”


 

Agizo hilo limepokelewa kwa furaha na shangwe kutoka kwa madiwani wa Jiji la Arusha waliokuwa wakihudhuria kikao cha mwisho cha Baraza la Madiwani, ambapo Waziri Mchengerwa pia alitoa pongezi kwa kazi kubwa iliyofanywa na madiwani hao katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi wao kwa wananchi.





“Ni kazi ya juhudi, ubunifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu. Nawapongeza mameya wote na madiwani kote nchini, hususan Meya wa Jiji la Arusha, kwa namna walivyowahudumia wananchi kwa moyo wa kujitolea.”


 

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alieleza wazi kuwa madiwani wametekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, huku akitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa malipo ya wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji yanafika moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi.

“Kuanzia sasa, ndani ya Mkoa wa Arusha, malipo ya wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji yatapelekwa moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi. Hili litapunguza usumbufu, kuondoa mianya ya rushwa na kuongeza uwajibikaji,” alisema Makonda.

Akiendelea na maelekezo yake, Makonda alisisitiza kuwa kila mwenyekiti wa mtaa au kitongoji apewe nakala ya bajeti ya mwaka husika na kwamba kila mradi wa maendeleo unapoanza, viongozi wa serikali lazima wapite kwa mwenyekiti wa eneo hilo kwa ajili ya kutoa taarifa rasmi.

“Tunataka ushirikishwaji wa kweli. Hatuwezi kuendelea kutekeleza miradi kwa siri. Mwenyekiti wa mtaa lazima awe na taarifa sahihi ya kinachoendelea kwenye eneo lake,” alisema Makonda.

Aidha, alihimiza viongozi hao kuwa mabalozi wa amani kuelekea uchaguzi mkuu, akieleza kuwa kata zote zinapaswa kubaki katika hali ya utulivu ili kulinda taswira ya mkoa wa Arusha kama kitovu cha utalii nchini.

“Twendeni tuwaambie wananchi juu ya kazi nzuri ya Rais Samia. Tusikubali kata zetu kuwa chanzo cha vurugu. Amani ya Arusha ni msingi wa uchumi wetu,” aliongeza.

Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, hakuhudhuria kikao hicho, licha ya kuwa ni kikao muhimu cha kuhitimisha muhula wa utumishi wa madiwani. 



Gambo, ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kwa muda mrefu ameonekana kuwa na mvutano wa wazi na baadhi ya madiwani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa sasa, Paul Makonda, hakutoa taarifa rasmi juu ya kutokuwepo kwake katika kikao hicho.



Kutohudhuria kwa Gambo kumeacha maswali hasa ikizingatiwa kuwa kikao hicho kilikuwa cha mwisho kwa baraza hilo na kilihudhuriwa na viongozi wa mkoa na wilaya akiwemo Waziri mwenye dhamana ambaye aliongea na madiwani kwa njia ya simu.

Kwa upande wake, Waziri Mchengerwa alihitimisha kwa kusema:



“Mafanikio tunayoyaona leo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Madiwani wameandika historia, na nina imani wengi wenu mtarejea kuendelea kuwatumikia wananchi.”


 

Makonda pia alitoa wito wa mshikamano na kuonya dhidi ya tabia ya baadhi ya viongozi kuwa chanzo cha migogoro.

“Kuna wengine mnaombeana mema, lakini kuna waliokuwa wanapigana vita kila siku, hadi hamna kitu cha maana kinachofanyika. Hili siyo jambo la kujivunia,” alisema.


 

Mkutano huo wa kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani umeacha alama ya maelekezo muhimu kwa taifa zima kuhusu uwajibikaji, ushirikishwaji wa wananchi na usimamizi wa haki na rasilimali katika ngazi ya msingi ya utawala.

0 Comments:

Post a Comment