AMRI YA KUTOTOKA NJE YATANGAZWA LOS ANGELES KUFUATIA MACHAFUKO

 


Meya wa jiji la Los Angeles, Karen Bass, ametangaza rasmi amri ya kutotoka nje katika juhudi za kukabiliana na hali ya uharibifu mkubwa unaoendelea kushuhudiwa jijini humo. Amri hiyo inaanza kutekelezwa kuanzia saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi na inatarajiwa kudumu kwa siku kadhaa.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meya Bass alisema kuwa uamuzi huo ni muhimu kwa ajili ya usalama wa wakazi wa jiji la Los Angeles. “Kumekuwa na uharibifu mkubwa katika jiji lote. Nitashauriana na viongozi waliochaguliwa na maafisa wa kutekeleza sheria kesho ... tunatarajia amri hii idumu kwa siku kadhaa,” alisema Bass.

Mkuu wa Polisi wa Los Angeles, Jim McDonnell, naye alieleza kuwa amri ya kutotoka nje ni hatua muhimu ya kuokoa maisha na kulinda mali za umma na binafsi. Alionya kuwa yeyote atakayekiuka amri hiyo atakamatwa bila upendeleo wowote.

Meya Bass pia alieleza wasiwasi wake juu ya matumizi ya nguvu ya kijeshi, akieleza kuwa hataki Rais Donald Trump kupeleka wanajeshi mitaani. “Nafikiria juu ya familia ambazo zinaogopa kwenda kazini na kwenda shule,” alisema kwa masikitiko.

Katika hatua nyingine ya kisheria, Jaji wa Marekani alizuia ombi la dharura kutoka kwa Gavana wa California, Gavin Newsom, lililokuwa likilenga kuzuia matumizi ya wanajeshi kushughulikia maandamano. Gavana Newsom alieleza kuwa hatua ya kutuma majeshi ni kinyume na sheria.

Hata hivyo, Rais Trump ametetea uamuzi wake, akisema kuwa hataruhusu jiji lolote la Marekani kuvamiwa na kutawaliwa na wahamiaji, na kwamba hatua hiyo ni ya kulinda usalama wa taifa.

Hali bado ni tete jijini Los Angeles huku wakazi wakiombwa kushirikiana na mamlaka kuhakikisha hali ya utulivu inarejea haraka iwezekanavyo.

0 Comments:

Post a Comment