Serikali ya Tanzania imepanga kuanzisha mpango wa kuuza sarafu za dhahabu kwa wananchi, ikiwa ni hatua ya kuwaongezea Watanzania njia mbadala za uwekaji akiba na uwekezaji kupitia dhahabu.
Akizungumza Mei 17, 2025 mkoani Geita wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya Stanbic, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema:
“Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tunajadiliana namna bora ya uanzishwaji wa sarafu za dhahabu ili kuongeza umiliki wa dhahabu miongoni mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu na mzunguko wa fedha ndani ya nchi yetu.”
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya mpango wa ununuzi wa dhahabu kupitia BOT ili kuhakikisha unakuwa endelevu na wenye tija kwa Taifa.
“Naziomba taasisi za fedha ziiangalie sekta ya madini kwa upekee na kuwawezesha Watanzania kimtaji ili washiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, kwani ina utofauti mkubwa na sekta nyingine za uzalishaji nchini,” alisema Mavunde.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic, Fredrick Maxi alisema:
“Benki ya Stanbic kwa sasa ina matawi 15 nchini na tunapanua huduma hadi maeneo ya wachimbaji. Tunakuja na mpango maalum wa kutoa mikopo kwa riba ndogo isiyo ya kibiashara kwa sekta ya madini, na wachimbaji wadogo sasa wanaweza kukopa hadi Shilingi Milioni 115 bila kuwa na dhamana.”
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela naye alitoa pongezi kwa hatua hiyo akisema:
“Hii ni matokeo ya kazi nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita. Ni fursa kwa wananchi wa Geita kutumia huduma za kifedha ili kujiimarisha kimtaji na kuchangia uchumi wa Mkoa.”
Mpango huu unatarajiwa kuchochea zaidi ushiriki wa wananchi katika soko la madini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.


0 Comments:
Post a Comment