Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa kauli kali dhidi ya kile alichokiita “uvamizi” wa wanaharakati kutoka nchi jirani, akisisitiza kuwa Tanzania haitakubali kuingiliwa katika masuala yake ya ndani.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya Willy Mutunga, na wanaharakati wengine wawili kuzuiwa kuingia nchini na kisha kurejeshwa Nairobi.
“Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku,” alisema Rais Samia alipokuwa akizindua toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), jijini Dar es Salaam.
Rais Samia aliendelea kusisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye utulivu na haitaruhusu watu kutoka nje kuiingiza kwenye machafuko. “Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu,” aliongeza.
Wakili Martha Karua, ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria nchini Kenya, alithibitisha kufurushwa kutoka Tanzania. “Nilizuiwa mara tu niliposhuka uwanja wa ndege na kisha kurejeshwa Kenya. Haikuwa na sababu halali isipokuwa kunizuia kuhudhuria kesi ya Tundu Lissu,” alisema Karua.
Wenzake, wakiwemo Mutunga na wanaharakati wengine, pia walirudishwa nchini kwao baada ya kuzuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. “Tulizuiwa kabla hata ya kuingia nchini. Hatukupewa maelezo yoyote ya kisheria kuhusu uamuzi huo,” alisema Mutunga.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Korir Sing’oei, ameitaka Tanzania kuheshimu haki za binadamu na misingi ya ushirikiano wa kikanda. “Nasisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa watu wa Afrika Mashariki kusafiri na kushiriki kwenye shughuli halali katika ukanda huu,” alisema Sing’oei.
Katika kauli kali iliyotolewa na Muungano wa Wanasheria wa Afrika (PALU), shirika hilo lililaani hatua ya kuwakataa wanaharakati hao, likisema ni kinyume cha mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tulizungumza nao na tumethibitisha kuwa walikamatwa bila sababu na kurejeshwa bila kupewa nafasi yoyote ya kujieleza,” alisema Donald Deya, Afisa Mtendaji Mkuu wa PALU. “Hili ni jambo la kushtua na la kuvunja haki za binadamu. Haki ya kushuhudia mashauri ya wazi ya jinai ni haki ya msingi iliyolindwa na Hati ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.”
Deya aliendelea kusema: “Tunaitaka Serikali ya Tanzania kuomba radhi kwa hatua hii isiyo halali, kutoa fidia kwa wahusika, na kutoa hakikisho kuwa wataweza kurejea kushuhudia kesi ya Tundu Lissu bila vikwazo.”
Kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, kiongozi wa upinzani kupitia chama cha CHADEMA, iliendelea Jumatatu katika Mahakama ya Kisutu, huku kukiwa na hali ya taharuki na ulinzi mkali. Lissu alishtakiwa mwezi uliopita, lakini amekanusha mashtaka hayo akiyaita ya kisiasa.
Karua, anayefahamika kwa msimamo wake wa kutetea haki, amesema: “Nimeshuhudia hali kama hii kabla. Nilimwakilisha Kizza Besigye nchini Uganda, naye pia alikumbwa na mashtaka ya kisiasa kama haya. Tunapaswa kupinga kwa nguvu zote juhudi za kunyamazisha upinzani.”
Hadi sasa, Serikali ya Tanzania haijatoa tamko rasmi juu ya tukio hilo, lakini kauli ya Rais Samia imeonekana kuashiria msimamo wake wa kutoruhusu kile alichokiita “watovu wa adabu” kuvuka mipaka ya Tanzania.
“Niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na ninyi wasimamizi wa sera zetu za nje, msitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kuvuka hapa kwetu,” alisisitiza Rais Samia.
Mataifa jirani na mashirika ya kimataifa yanatazama kwa makini mwenendo wa kesi ya Tundu Lissu na hali ya haki za binadamu nchini Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.


0 Comments:
Post a Comment