Uteuzi wa Ng'ang'a ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo Mei 6, 2025, ambapo alichukua nafasi ya Dadi Horace Kolimba aliyehamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga.
Akizungumza mara baada ya kumuapisha, Paul Makonda alimtaka Ng'ang'a kuendelea kujituma kwa bidii na kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo kwa wilaya ya Karatu.
Alisema:
“Ninakupongeza kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu. Umeaminiwa kutokana na uadilifu na utendaji wako. Karatu ni eneo lenye changamoto na fursa nyingi, hivyo nataka kuona ushirikiano na kasi ya maendeleo ikiongezeka.”
Kwa upande wake, Lameck Ng'ang'a alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, weledi na mshikamano na viongozi wenzake katika ngazi zote.
Alisema:
“Ninamshukuru Rais kwa kuniamini na kunipa jukumu hili kubwa. Nitajitahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa dini, siasa, watumishi wa umma na wananchi wote wa Karatu ili kuhakikisha tunaleta maendeleo ya kweli.”
Ng'ang'a aliwahi kuwa Katibu Tarafa wa Karatu kabla ya 2023 alipoteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu ambapo sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, jambo ambalo linaelezwa kumpa faida ya kuijua vema wilaya hiyo na changamoto zake.
Uapisho huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa, wilaya pamoja na wawakilishi wa taasisi za serikali, huku ukitafsiriwa kama mwanzo mpya wa msukumo wa maendeleo katika Wilaya ya Karatu.









0 Comments:
Post a Comment