Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameonesha dhamira ya serikali katika kufufua viwanda vilivyokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa kushirikiana na uongozi wa Shirika la Nyumbu katika ziara maalum ya kutathmini hali ya Kiwanda cha General Tyre kilichopo jijini Arusha.
Ziara hiyo imelenga kurejesha matumaini kwa wakazi wa Arusha kupitia mpango wa serikali wa kufufua viwanda vilivyojenga historia ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania. Akiwa katika kiwanda hicho, Makonda alisema:
“Tunataka kuona namna gani tunaweza kufufua kiwanda hiki, ambacho ni tumaini kwa wananchi wa Arusha. Lengo letu ni kuhakikisha viwanda kama General Tyre vinafufuliwa kwa ushirikiano wa karibu na taasisi za umma na binafsi.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumbu, Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Yusuph Kisamba, alisema kuwa hatua za awali zimeanza kuchukuliwa ili kuwekeza katika kiwanda hicho kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara:
“Shirika linaangalia uwezekano wa kuwekeza katika kiwanda hiki kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, na tayari tumeshafanya tathmini ya awali ya miundombinu na mahitaji muhimu kwa ajili ya uendelezaji wa kiwanda.”
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumbu, Kanali Charles John Kalambo, alieleza kuwa shirika lake liko tayari kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani:
“Shirika lipo tayari kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama matairi, pasi aina ya Philips na vifaa vingine vya viwandani, kulingana na mahitaji ya soko la ndani na taasisi za serikali kama halmashauri na wizara mbalimbali.”
Mshauri wa kiufundi wa Shirika la Nyumbu, Mhandisi Juma Kassim Kumbikila, alieleza kuwa mazingira ya kiwanda bado yako katika hali nzuri na yanaweza kutumika kwa upanuzi wa uzalishaji:
“Eneo la ekari 50.4 lililokuwa likitumika na General Tyre bado lipo katika hali nzuri na linaweza kutumika kwa upanuzi wa uzalishaji.”
Mpango wa kufufua kiwanda hiki unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi mkoani Arusha, kutoa fursa za ajira kwa vijana, na kuimarisha uzalishaji wa viwandani nchini. Serikali inatarajia kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali ili kufanikisha azma hii.





0 Comments:
Post a Comment