Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa CWT anayekaimu nafasi hiyo kwa sasa, Mwalimu Joseph Misalaba alisema:
“Mkutano huu wa saba wa kitaifa unakuja baada ya kukamilika kwa chaguzi za ngazi ya shule, wilaya na mkoa. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha uongozi mpya wa kitaifa unapatikana kwa mujibu wa katiba ya chama.”
Taarifa rasmi ya chama hicho iliyosainiwa na Afisa Habari na Mahusiano wa CWT imethibitisha kuwa mbali na nafasi ya Urais, ambayo imevutia wagombea 18, kutakuwa pia na uchaguzi wa nafasi nyingine muhimu za uongozi.
Afisa huyo alieleza:
“Nafasi zinazogombewa ni pamoja na Rais wa chama, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mweka Hazina. Pia kutakuwa na wawakilishi wa walimu wanawake, walimu walemavu, walimu vijana pamoja na Wadhamini wa chama.”
Mkutano huo wa kitaifa unatarajiwa kuwakutanisha walimu kutoka mikoa yote ya Tanzania, ambapo pamoja na uchaguzi, masuala muhimu ya maendeleo ya walimu yatajadiliwa, ikiwa ni pamoja na ustawi wa taaluma ya ualimu, mazingira ya kazi, na maslahi ya wanachama wa CWT.
Chama cha Walimu Tanzania kimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na maslahi ya walimu, hivyo uchaguzi huu unaonekana kuwa wa kihistoria kwa kuzingatia idadi kubwa ya wagombea na umuhimu wa nafasi zitakazojazwa.
Walimu na wadau wa sekta ya elimu wanatazama kwa karibu uchaguzi huu, wakitarajia kupata viongozi wenye maono, weledi na dhamira ya kweli ya kuendeleza mafanikio ya CWT na kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya walimu nchini.

0 Comments:
Post a Comment