KONGAMANO LA UCHUMI LA ARUSHA: DIRA MPYA YA MAENDELEO SHIRIKISHI NA UWEKEZAJI WA KISASA

 


Ametaka ongamano hilo liwe chachu ya kufungua milango mipya ya uwekezaji kwa kushirikisha Wizara na Taasisi zote husika za Serikali ili kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yanaboreshwa kwa wepesi, uwazi na ushawishi chanya.





Katika Kongamano la Uchumi la Arusha lililofanyika Mei 3, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejizatiti kuwasogezea wananchi maendeleo kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.



Akizungumza kama mmoja wa watoa mada wakuu katika kongamano hilo, Mchengerwa alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuwakomboa wananchi kutoka katika mnyororo wa ukosefu wa taarifa, huduma na fursa kwa kuwawekea mazingira bora ya kupata maarifa, miundombinu na uwezo wa kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao.


"Tupo katika zama ambazo maendeleo hayategemei tena maamuzi ya viongozi wa kitaifa peke yao, bali yanategemea uwezo wa maeneo yetu ya mikoa na halmashauri zetu kuongoza kwa dira, maarifa na maamuzi ya kimkakati," alieleza.



Akaongeza kuwa, "Utawala bora siyo tu matumizi ya sheria bali ni falsafa ya kuwezesha kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika ndoto ya taifa na kujenga taasisi imara, kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na kutoa huduma kwa usawa bila upendeleo."



Kupitia sera ya Decentralization by Devolution (D-by-D), Serikali imeziwezesha halmashauri kupanga na kutekeleza mipango yao kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi wao, hali inayolenga kukuza demokrasia ya kiuchumi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.



"Kwa maana hiyo, TAMISEMI imewapa halmashauri zetu nguvu ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa mazingira ya jamii zao. Hili linawezesha uwekezaji wa ardhi, huduma bora kwa wananchi, na kuimarisha mapato ya ndani," alifafanua.



Mchengerwa alisisitiza kuwa maendeleo ya mikoa hayawezi kuletwa na mipango ya makaratasi pekee bali yanahitaji uthubutu wa viongozi wa ngazi za chini kutambua changamoto halisi, kufanya tafiti za kina na kuanzisha ushirikiano mtambuka baina ya sekta mbalimbali kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya taifa.



Alielekeza kuwa maeneo yaliyotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya uwekezaji yaharakishwe kuhuishwa kwa kupangwa kitaalamu, kupimwa kwa usahihi, fidia kutolewa kwa haki, na miundombinu ya msingi kujengwa kwa kasi na ubora.



Aidha, alitaka ushirikishwaji wa wananchi ufanyike kwa kina na kwa uwazi bila ubaguzi wowote wa kijinsia, hali ya kiuchumi, mila wala hadhi, huku akisisitiza kuwa wakulima, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo wanapaswa kuwa sehemu ya msingi ya mchakato wa maendeleo.

"Ustawi wa mikoa hautatokana na maazimio ya makaratasi pekee, bali na uthubutu wa viongozi wake kuondoa matabaka baina ya walionacho na wasio nacho," alisema na kuongeza kuwa ni lazima kutumia teknolojia ya kisasa na maarifa ya ndani ili kubuni uwekezaji wa kisasa wenye tija na ustahimilivu wa muda mrefu.


Alihitimisha kwa kutoa wito kuwa Kongamano la Uchumi la Arusha liwe ni chemchemi ya fikra mpya, dira ya uwekezaji na mlango wa fursa kwa kila raia wa mkoa wa Arusha, awe kijijini au mjini.


0 Comments:

Post a Comment