Mtambo wa ATC Kuziba Pengo la Umeme Kaskazini na Kuokoa Fedha za Kigeni Ifikapo Novemba 2026

🚨Bilioni 38 Kuanzisha Mapinduzi ya Nishati Kikuletwa: 


📍Mtambo wa ATC Kuziba Pengo la Umeme Kaskazini na Kuokoa Fedha za Kigeni Ifikapo Novemba 2026


📌Kuondoa Uhaba wa Wataalamu



Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza shilingi bilioni 38 katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) Kampasi ya Kikuletwa ili kuondoa kabisa uhaba wa wataalamu wa nishati jadidifu nchini. 


Mradi huu mkubwa wa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa nguvu ya maji (Hydropower) unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Novemba 2026, huku ukilenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Kanda ya Kaskazini.



Mratibu wa Mradi wa EASTRIP kutoka ATC na Kaimu Meneja wa Kampasi ya Kikuletwa, Mhandisi Sithole Mwakatage, amebainisha kuwa uwekezaji huo unajenga Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu kitakachotumia mfumo wa kisasa wa ujifunzaji kwa vitendo.


Aliyasema hayo wakati wajumbe wa Kamati Tendaji ya Usimamizi na Uongozi wa Mradi wa Kuendeleza Ujuzi (EASTRIP) walipotembelea kituo hicho kilichopo Hai mkoani Kilimanjaro leo Mei 14, 2025.


"Tumejenga kituo cha kufua umeme wa maji chenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.65, ambacho kina dhana ya 'Factory for Teaching' (Kiwanda cha Kufundishia). Wanafunzi wanajifunza kwa vitendo kuanzia siku ya kwanza wanapoingia chuoni," alisema Mhandisi Mwakatage.


Teknolojia ya Kipekee Kusafisha Gridi ya Taifa



Mhandisi Mwakatage alieleza kuwa mtambo huo una upekee mkubwa wa kiteknolojia ukilinganisha na mitambo mingine nchini, kwani una uwezo wa kujiwasha wenyewe bila kutegemea nguvu ya gridi ya taifa wakati wa dharura (Black Start capability).

"Ni mtambo wa kisasa unaotegemea betri, na mfumo wake wa msisimko (excitation system) unatumia umeme kutoka vyanzo vya betri na kuanza kufua umeme. Mtambo huu uko kimkakati kuisaidia gridi pale inapokuwa imefeli," alifafanua Mwakatage.



Mradi huu unaenda kutatua changamoto ya muda mrefu ya mdororo wa voltage katika Kanda ya Kaskazini, hatua itakayookoa fedha za nchi zilizokuwa zikitumika kununua umeme nje ya nchi.

"Hapo awali, serikali ilikuwa imelazimika kununua umeme kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kuimarisha voltage (Voltage Stabilization), lakini sasa uwepo wa mtambo huu unaenda kupunguza au kuondoa kabisa tatizo hilo."

Malengo Makuu na Hatua za Utekelezaji





Naye Mhandisi wa ATC anayesimamia mradi huo eneo la Kikuletwa, Mhandisi Adam Mfangavo, alieleza kuwa mradi una malengo makuu mawili: kutumika kama kituo cha umahiri cha mafunzo, uzalishaji, na ukarabati wa mifumo ya hydropower, pamoja na kuzalisha umeme utakaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia shirika la TANESCO.

Mhandisi Mfangavo alifafanua kuwa mradi unatekelezwa katika awamu mbili:



Awamu ya Kwanza: Ujenzi wa majengo mawili na ufungaji wa mitambo ulikamilika rasmi Machi 2026.



Awamu ya Pili: Imeanza mwezi huu wa Mei 2026 na itachukua miezi sita hadi kukamilika kwake Novemba 2026.


"Novemba mwaka huu, mradi utaanza kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 1.65, unaoweza kutosha kulisha umeme magorofa 100. Mtambo ukitengeneza umeme utaanza kusambaza kwenye gridi ya taifa na pia kutumika kwa ajili ya ufundishaji," alisema Mhandisi Mfangavo.

Mradi huu tayari unanufaisha jamii inayozunguka kituo kwa kupata fursa za ajira, huku wanafunzi wa fani za Hydropower, Nishati Jua (Solar), Mitambo (Mechanical), na Umeme wakipata mafunzo ya vitendo (Industrial Practical Training).

Kupaa kwa Idadi ya Wanafunzi na Miundombinu Mpya



Kutokana na maboresho haya, Kampasi ya Kikuletwa inajipanga kupokea ongezeko kubwa la wanafunzi kutoka 70 wa awali hadi kufikia 600 mara mradi utakapoanza kazi. Chuo kimejenga kampasi mpya yenye madarasa, karakana (workshops), na mabweni ya kutosha.



Katika hatua ya kipekee, chuo kimejenga hosteli maalum kwa ajili ya wanafunzi watu wazima wenye watoto ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo. Mbali na nishati ya maji, kuna mipango ya kupanua kituo hicho ili kuwa na mashamba ya nishati ya jua (Solar Farm), nishati ya upepo (Wind Power), na nishati ya biogas ili kukifanya kuwa kituo kamili cha umahiri katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.


Wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wameonyesha kuridhishwa na uwekezaji huo mkubwa unaowapa fursa ya kujifunza kwa vitendo na mazingira bora ya chuo.



"Ninaridhishwa sana na mafunzo yanayotolewa hapa chuoni pamoja na mandhari nzuri sana ya chuo hiki," alisema Christina Mushi, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesomea fani ya Mabomba (Plumbing).



Naye mwanafunzi mwenzake, Paulo Ngoyaine, aliongeza kuwa: "Chuo kiko vizuri sana na mafunzo yake yanatolewa kwa vitendo zaidi, jambo linalotujengea uwezo mkubwa."



Kukamilika kwa mradi huu kunatajwa kuwa mkombozi wa soko la ajira nchini, kwani utazalisha nguvu kazi maalum (workforce) itakayosaidia kuendesha miradi mingine mikubwa ya kimkakati kama ule wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), ambalo linahitaji wafanyakazi wataalam zaidi ya 2,000 kwa wakati mmoja.


Mradi wa EASTRIP ni wa kikanda unaotekelezwa katika nchi za Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa Tanzania, mradi huo unahusisha ujenzi na uimarishaji wa vituo vya umahiri katika vyuo vitatu vikuu: Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Dar es Salaam (DIT), na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Vituo hivyo vinatarajiwa kutoa mafunzo ya kitaalamu na ya vitendo katika sekta za nishati jadidifu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchakataji ngozi, pamoja na usafirishaji wa anga. 


Hatua hii inalenga kuongeza ujuzi wa vijana na kuimarisha ushindani wa kikanda katika soko la ajira. 

0 Comments:

Post a Comment