Usambazaji Gesi Asilia Majumbani Waanza Lindi- TPDC



Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeendelea kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanzisha utekelezaji wa mradi wa usambazaji gesi asilia majumbani katika mikoa ya Lindi na Pwani. Mradi huu unalenga kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia, hivyo kupunguza utegemezi wa nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira kama mkaa na kuni.

Utekelezaji wa Mradi na Maendeleo Yake

Meneja wa Mradi wa Usambazaji wa Gesi Asilia Majumbani, Tumaini Daniel, alieleza kuwa serikali imeendelea kutenga fedha za kutekeleza mradi huu ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetengwa kwa ajili ya usambazaji wa gesi asilia katika maeneo ya Lindi (Mnazi Mmoja) na Pwani (Mkuranga). Aidha, Tumaini alisema kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 38.18 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2025.

"Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na unahusisha ujenzi wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwa nyumba 980 (Nyumba 529 za Mkuranga – Pwani na nyumba 451 Mnazi Mmoja – Lindi)," alifafanua Tumaini. Mtandao wa gesi asilia utawekwa kwa urefu wa kilomita 47.86, ambapo kilomita 22.9 zitakuwa mkoani Lindi na 24.96 zitakuwa mkoani Pwani.

Faida za Gesi Asilia

Tumaini alisisitiza kuwa matumizi ya gesi asilia ni njia bora na nafuu kwa wananchi, kwani ni rafiki wa mazingira, inaokoa muda, na inapatikana wakati wote. Alitoa wito kwa wananchi kutumia nishati hii ipasavyo pindi mradi utakapokamilika, akionya dhidi ya kuendelea kutumia nishati zinazochangia uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa hali ya hewa.

"Wito wangu kwa wananchi ni kutumia gesi asilia hii kwa manufaa yao, kwani ni gharama nafuu na inachangia katika uhifadhi wa mazingira," alisema Tumaini.

Ushirikiano wa Wananchi katika Utekelezaji wa Mradi

Afisa Maendeleo ya Jamii, Oscar Mwakasege, alisisitiza kuwa TPDC itaendelea kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa mradi huu kupitia majukwaa mbalimbali ya elimu kama mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, makongamano, na michezo. Alisema kuwa zoezi la utoaji elimu kuhusu mradi ni endelevu na kila hatua ya mradi wananchi hushirikishwa ili kuhakikisha ufanisi wa mradi na kulinda miundombinu ya gesi asilia.

"TPDC imeendelea kuwasiliana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara, elimu kupitia vyombo vya habari na nyumba kwa nyumba ili kujenga uelewa wa mradi kwa wananchi, na kuhakikisha usalama wa miundombinu ya gesi," alisema Oscar.

Fursa za Ajira kwa Wananchi

Mradi huu pia umeleta fursa za ajira kwa wananchi. Bi. Hawa Fumau Dadi, mkazi wa Mtaa wa Mnazi Mmoja na mnufaika wa ajira katika mradi wa gesi asilia, aliishukuru TPDC kwa kutoa fursa za ajira zinazowasaidia wananchi kutimiza mahitaji yao ya kila siku.

"Nashukuru kwa kupata kazi katika mradi huu wa TPDC katika mtaa wa Muungano mnazi mmoja, tunashukuru tumepata ajira inayotuwezesha kupata fedha za kuendesha maisha ya kila siku," alisema Bi. Hawa.

Mchango wa Diwani na Wananchi

Diwani wa Kata ya Mnazi Mmoja, Said Mohammed Mchinjita, alitoa shukrani kwa TPDC kwa kuendeleza mradi wa usambazaji gesi asilia katika kata hiyo na kuhimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu na kuimarisha ulinzi na usalama wa miundombinu ya mradi.

"Ni muhimu wananchi tushirikiane na wataalamu na kuimarisha ulinzi na usalama wa mali na vifaa vya wakandarasi ili mradi huu ukamilike kwa wakati," alieleza Mchinjita.


Serikali kupitia TPDC itaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa kutenga fedha kwenye bajeti ya maendeleo ya kila mwaka. Mradi huu wa usambazaji gesi asilia majumbani unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, kuleta mabadiliko chanya katika matumizi ya nishati na kuchochea maendeleo endelevu katika maeneo ya Lindi na Pwani.

0 Comments:

Post a Comment