Showing posts with label nishati. Show all posts
Showing posts with label nishati. Show all posts

 


Happy Lazaro,Arusha.


Wananchi wametakiwa kutumia bidhaa za umeme jua kutoka kampuni ya teknolojia ya  ZOLA ELETRIC kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwani  bidhaa hizo  zina ubora wa hali ya juu .



Hayo yamesemwa  jijini Arusha na Afisa masoko wa kampuni hiyo Moses Vikael wakati akizungumza katika mbio za Redcross Marathon Arusha zilizofanyika katika uwanja wa Stadium jijini Arusha .



 "Tunafanya kazi ya uuzaji na usambazaji wa sola katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mtandao wa mawakala wetu, kuanzia mijini hadi vijijini, na katika sekta zote za biashara, taasisi na makazi ya wananchi."amesema Moses.



"Lengo letu ni kuhakikisha kila eneo lenye uhitaji wa nishati linapata suluhisho bora la umeme wa jua kutoka kampuni yetu "amesema Moses.



Moses ameongeza  kuwa,kitendo hicho kilichofanywa na Redcross ni mfano wa kuigwa kwani kwa mara ya kwanza wameweza kufanya mbio hizo kwa mkoa wa Arusha jambo ambalo limeweza kuleta hamasa kubwa kwa wananchi wa Arusha .


"Tunashukuru sana kwa namna ambavyo.Redcross mmeweza kutupa mwaliko wa kuwa wafadhili katika jambo hili na tunawaahidi kuendelea kushirikiana na nyie katika kila hatua "amesema  Moses.



Aidha ametoa wito kwa wananchi mbalimbali kiwa na tamaduni za kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao kwani michezo ni afya na inasaidia kuondokana na maradhi mbalimbali ambayo yangeweza kutokea .







Happy  Lazaro,Arusha .

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude,amezindua rasmi chapa yake  mpya ya gesi safi ya kupikia, LOTI GAS,huku akisisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi kwa maendeleo ya afya, mazingira na uchumi wa wananchi.



Aidha Mkuu wa wilaya  huyo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wananchi hao kutumia nishati hiyo kwa wingi ili kutunza mazingira .




Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkude ameipongeza kampuni ya LOTI GAS kwa uwekezaji wake ambao amesema unaenda sambamba na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda mazingira pamoja na afya za wananchi.


Mkude amesema mwitikio wa matumizi ya nishati safi nchini umefikia asilimia 28.6, huku juhudi mbalimbali zikiendelea kuhakikisha taifa linafikia malengo yaliyojiwekea katika sekta hiyo muhimu.


"Uwekezaji wa kampuni ya LOTI GAS umefungua fursa za ajira kwa vijana na kuchangia kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha pamoja na taifa kwa ujumla."amesema Mkude .


Aidha ameihimiza menejimenti na watumishi wote wa LOTI GAS kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama, ubora wa bidhaa pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja ili kujenga imani kwa wananchi.


"Nawasihi wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya matumizi ya nishati safi, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia njema ili kuweka mazingira bora ya biashara na maendeleo nchini."amesema Mkude .



Akizungumza kwenye uzinduzi huo ,Mkurugenzi wa Loti Energies, Collins Kimaro amesema kuwa , dira ya kampuni hiyo ni  kuona Tanzania ambayo kila nyumba—kuanzia  Arusha hadi maeneo ya vijijini—inaweza kutumia nishati safi ya kupikia kwa usalama, kwa upatikanaji rahisi na kwa gharama  rafiki.


Aidha amefafanua kuwa ,  tofauti ya Loti Gas ni kwamba inakuletea amani kwani  afya inalindwa kwa sababu hamna moshi,mitungi misafi na mipya na amani kutokana na usalama, imepimwa na ina vigezo vyote na ni bei rafiki.



Aidha ameongeza kuwa,gas hiyo inapatikana kwa urahisi, madukani au kwa delivery .ambapo mteja anapelekewa sehemu yoyote .



"Uzinduzi huu umefanyika chini ya kampeni ya “Tupo Jikoni na Loti – Gesi ya 

Kuaminika Kwako”, ambapo uzinduzi huo  umeambatana na shindano la kupika supu lililoonyesha  matokeo mazuri na ladha ya kuvutia, kuthibitisha ubora wa Loti Gas katika matumizi ya kila siku."amesema  Mkurugenzi Kimaro.




Uzinduzi huo ambao umefanyika katika ukumbi wa  Aim Mall Arusha ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ambao kwa pamoja  wamepongeza kampuni ya Loti Energies kwa uwekezaji huu inayounga mkono malengo ya serikali ya kuendeleza nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wote.



"Uzinduzi ulionyesha pia uwepo wa wakala wengi wa Loti Gas, jambo linalothibitisha 

kuwa tayari Loti Gas imeanza kupatikana sokoni Arusha, ikiwa na mitungi ya kilo 6 na 

kilo 15, na mpango wa kupanua zaidi kadri mahitaji yanavyoongezeka."amesema Kimaro.






Happy Lazaro,Arusha 



KAMPUNI   ya nishati jua inayoongoza duniani ya Sun King  imezindua nembo yao mpya iliyoboreshwa  zaidi ambapo  hatua hiyo  kubwa inayodhihirisha ukuwaji wa kampuni hiyo. 




Aidha kupitia uzinduzi wa nembo hiyo mpya, Sun King  yenye kauli mbiu ya "Angaza Maisha Yako" itaendelea kutoa huduma bora za kimataifa ili kuhakikisha wateja wake wanapata  huduma hizo kwa uhakika na ukaribu zaidi. 




"Hii inadhihirika kupitia kampeni yao mpya ya "PATA ZAIDI "ambayo inalenga ,Uokoaji zaidi –Kupitia bidhaa bora na za bei nafuu kutoka Sun King,Utulivu wa akili zaidi kupitia huduma zao bora."amesema Anish .




Ameongeza kuwa ,kampeni hiyo pia inalenga katika Chaguo zaidi  kwa bidhaa zao ndogo za taa hadi bidhaa kubwa za inverter zenye uwezo mkubwa  pamoja na Nishati ya kuaminika zaidi   kwa nyumba, biashara na taasisi.


 


 "Nembo yetu iliyoboreshwa inaonyesha dhamira yetu kwa wateja wetu  kuendelea kutoa huduma za sola za bei nafuu majumbani na kwenye biashara, vifaa zaidi vinavyorahisisha maisha, na nguvu zaidi ya kukuza biashara, shule na jamii kwa ujumla,


Mmoja wa waanzilishi wa  kampuni hiyo ya Sun King  Anish Thakkar, amesema kuwa Safari ya  maboresho ya chapa yetu ya Sun King ni sehemu moja tu ya mageuzi mapana, na wana bidhaa kabambe zinazoguza maisha ya kawaida ya Watanzania zikiwemo,Mifumo ya jua ya HomePlus na HomePlus Pro ambayo hutoa mwanga wa kuaminika kwa kaya pamoja na kuchaji simu.




"SunKing imefunga sola zake kwa kaya zaidi ya milioni 24 huku zaidi ya kaya 300,000 mpya zikiunganishwa kila mwezi barani Afrika."amesema Anish .




Anish amefafanua  kuwa ,bidhaa kubwa za sola ziitwazo “inverter system” mbadala wa jenereta zinazopunguza matumizi ya umeme au mafuta hadi asilimia 80 pamoja  na simu mahiri za kijanja ambazo wateja wanaweza kulipia taratibu kwa malipo ya awamu.




Amefafanua kuwa, kampuni hiyo ina uzoefu wa kutosha katika sekta hiyo ya nishati ya jua ambapo kwa mara ya kwanza kabisa kumhudumia.mteja wa kwanza ilikuwa mwaka 2009 na hatimaye kuanzia hapo kampuni hiyo ikawa chachu ya kubadili maisha ya watu wengi duniani. 




Anish amefafanua kuwa, wameendelea kuwa kutoa suluhisho endelevu kwa mamilioni ya watu ambapo hadi kufikia sasa wapo katika zaidi ya nchi 65 duniani.




"Ikumbukwe kuwa watu takribani bilioni 1.8 duniani wanaishi bila nishati ya uhakika ,na kati ya hao kuna watanzania takribani milioni 13 ambao ni sawa na asilimia 22 ya watanzania wote ,sisi SunKing hatuwezi kukubali hali hii kuwa ni ya kawaida ,hivyo tunafanya kila jitihada kuhakikisha kila mwenye uhitaji anapata bidhaa zetu ambazo zimetengezwa kwa  ubunifu na ubora wa hali ya juu."amesema Anish.




"Tunapokwenda kusherehekea hatua hii muhimu ya uzinduzi wa chapa mpya ya SunKing ifahamike kuwa nembo yetu iliyoboreshwa inaonyesha dhamira yetu kwa wateja wetu kuendelea kutoa huduma za sola za bei nafuu majumbani na kwenye biashara, vifaa zaidi vinavyorahisisha maisha ,na nguvu zaidi ya kukuza biashara 




Katika uzinduzi huu wa chapa hii mpya iliyoboreshwa,Sun King inaendelea kusimamia dhamira yake ya kuangaza maisha ya Watanzania sasa na katika siku zijazo.




Kwa upande wake mgenirami katika uzinduzi huo   Dokta Mfawidhi kituo.cha Afya Themi,Dokta Charles  Sululu  ,amesema kuwa, kampuni ya Sun King ni ya kimataifa inayotoa huduma za nishati  jua ambayo imewekeza nchini ikiwa imedhamiria kufikisha nishati ya umeme wa jua kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa gridi ya taifa na sehemu zenye umeme wa gridi ya taifa  ili kuchangia kukuza uchumi wa nchi sambamba na maendeleo ya wananchi.


" nimefurahi kusikia kuwa kampuni kupitia sera yake ya uwajibikaji kwa jamii imeendelea kutoa misaada ya mitambo ya nishati ya umeme kwenye taasisi tofauti vikiwemo kwenye vituo vya aafya"amesema .




Ameongeza kuwa ,Kituo cha Afya cha Themi ni moja wapo ya wanufaika wakubwa wa juhudi hizo ambapo waliwapatiwa mtambo wa umeme jua  ambapo tangu wamepata msaada wa bidhaa yao  ya Solar inverter kumekuwa na ahueni mkubwa katika utoaji huduma za afya kwa mama na mtoto na wananchi wa Arusha kwa ujumla.


Dokta Sululu amesema kuwa , kupitia uwekezaji huo  wananchi mbali mbali watanufaika kupata bidhaa za nishati jua kwa gharama nafuu pamoja na kupata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.


"Nimesikia kuwa moja ya agenda ya mradi huu ni kufanikisha utunzaji wa mazingira kupitia kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama.ambapo aliwahimiza kuendelea na uwekezaji huo wa kuwezesha wananchi kujiletea maendeleo,kama ambavyo wengi wetu mnajua sehemu ikiwa na umeme,maisha ya wananchi yanakuwa bora kuliko maeneo yasiyo na umeme.


"Niwaombe pia kuendelea na jitihada za kushirikiana na vituo vya afya mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa mitambo yenu inaendelea kutumika katika kuchangia uboreshaji wa afya ya mama na mtoto."





 


Na Mwandishi Wetu, Tanga


Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP kupitia mkandarasi wake Besix Ballast Nedam (BBN) imetoa ufadhili wa mafunzo stadi kwa   wakazi 12 wa Kata ya Chongoleani panapojengwa miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta ghafi, hii ikiwa ni sehemu ya kuwajengea wananchi hao uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa ili kuwainua kiuchumi.


 


Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya ‘Local Content’ inayolenga kuwawezesha Watanzania kunufaiika na miradi mikubwa ya maendeleo.



Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo iliyofanyika chuoni hapo jijini Tanga, Meneja wa Kuijengea Uwezo Jamii wa EACOP, Martha Makoi, alisema kuwa mradi huo si tu unahusika na ujenzi wa bomba la mafuta, bali pia unalenga kuacha alama ya maendeleo kwa Watanzania kupitia uwezeshaji wa rasilimali watu na uboreshaji wa huduma za kijamii.


“Mradi huu ni wa kimkakati na unalenga kuwajengea uwezo Watanzania kupitia mafunzo, ajira na uboreshaji wa huduma,”



“Hadi sasa zaidi ya wanafunzi 200 wamefaidika na mpango huu kupitia mafunzo ya VETA na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadhi yao wamepewa ufadhili wa kusoma nje ya nchi,” alisema Makoi.




Naye Meneja wa Rasilimali Watu wa BBN,  Harry Mangowi, alisema kuwa wakazi hao 12 wamefadhiliwa kusomea fani za Useremala, Ushonaji, pamoja na Ususi na Urembo, ili waweze kujiajiri na kuisaidia jamii yao.


“Mbali na kutoa ajira, tumeona ni vyema kuwajengea uwezo kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujitegemea,” amesema Mangowi.



Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo hicho, Gideon Lairumbe, alisema kuwa ushirikiano kati ya VETA na EACOP umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu mafunzo hayo.


“Tunashukuru EACOP na BBN kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika mafunzo haya. Wanafunzi wanapopata mafunzo ya nadharia na vitendo, wanakuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na taasisi mbalimbali, hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alisema Bw. Lairumbe.


Mbali na ufadhili wa vijana, mkuu huyo pia ameishukuru EACOP kwa kutoa mafunzo kwa walimu wa chuo hicho na kuwezesha rasilimali vifaa vya kufundishia.


Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Chongoleani, Bw. Mohamed Salim, aliishukuru EACOP na mkandarasi BBN kwa kuendelea kutoa fursa za mafunzo na ajira kwa wananchi wa kata hiyo yenye vijiji vinne.


“Tunashuhudia jinsi mradi huu unavyonufaisha jamii yetu. Mbali na kunufaika na ajira zisizohitaji ujuzi, vijana wetu pia wanapewa nafasi ya kupata mafunzo ya ufundi ambayo yanawawezesha kujitegemea,” alisema.


Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Bi. Fatma Salim kutoka Kijiji cha Ndaoya, alisema kuwa kabla ya kupata ufadhili alikuwa hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, lakini sasa ana matumaini makubwa ya kujiajiri kupitia fani ya ususi na urembo.


Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Peninsula ya Chongoleani, mkoani Tanga, na unapita katika mikoa minane nchini Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Mradi huo unahusisha jumla ya wilaya 24, kata 134 na zaidi ya vijiji 180.


Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (62%), Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta Uganda (UNOC) kila moja ikiwa na asilimia 15, na Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya China (CNOOC) yenye asilimia 8.



 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amezindua rasmi teknolojia ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji inayojulikana kama High-Intensity Focused Ultrasound (HIFU) katika Hospitali ya Kairuki, Dar es Salaam. Uzinduzi huu ni wa kwanza kufanyika katika Afrika Mashariki na Kati.




Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Agosti 27, 2025, Dkt. Biteko amesema huduma hiyo ni hatua kubwa kwa taifa na inadhihirisha kasi ya maendeleo katika sekta ya afya nchini.

"Ni teknolojia ya kipekee ambayo itarahisisha maisha ya Watanzania wengi na pia kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi. Tanzania sasa ni miongoni mwa mataifa manne barani Afrika yanayotoa huduma hii, pamoja na Misri, Nigeria na Afrika Kusini," amesema Dkt. Biteko.



Aidha, ameipongeza Hospitali ya Kairuki kwa kutoa punguzo la asilimia 50 kwa wagonjwa 50 wa kwanza watakaopata huduma hiyo kwa mwezi wa mwanzo.

"Hii ni ishara ya upendo na kujali, lakini pia ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya kutoa huduma nafuu kwa wananchi," amesema.



Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za afya, huku akiwaasa watendaji wa Wizara ya Afya kuwa na moyo wa kujifunza.

"Watendaji wa wizara wasiogope kujifunza pale sekta binafsi inapofanya vizuri. Lengo letu sote ni moja — huduma bora kwa wananchi," amesisitiza Dkt. Biteko.



Dkt. Mwinyikondo Amir kutoka Wizara ya Afya, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, amesema:
"Tukio hili linaonesha wazi mshikamano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za kisasa."


Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Afya na Elimu Kairuki, Kokushubila Kairuki, ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa sekta binafsi.
"Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya afya imepiga hatua kubwa. Tutaendelea kuunga mkono juhudi hizi kupitia Dira ya 2050," amesema.

Ameeleza kuwa uwekezaji wa teknolojia ya HIFU umegharimu shilingi bilioni 12 na milioni 300, na hadi sasa wagonjwa 303 wamepatiwa huduma ya uchunguzi huku 298 wakipata matibabu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kairuki, Dkt. Onesmo Kaganda amesema:
"Uzinduzi wa HIFU ni tukio la kihistoria. Teknolojia hii ni suluhisho la matatizo ya uvimbe kwa kutumia mawimbi ya sauti bila kufanyiwa upasuaji."

Amefafanua kuwa HIFU inatibu uvimbe mbalimbali ukiwemo wa saratani na usio wa saratani katika maeneo kama matiti, kongosho, kizazi na tezi dume, huku faida zake zikiwa ni pamoja na kutoacha kovu, mgonjwa kutopasuliwa, kupona haraka na kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi.

Dkt. Kaganda ameongeza kuwa huduma hiyo pia husaidia kuboresha matokeo ya dawa za saratani, kupunguza kasi ya ukuaji wa saratani na kupunguza maumivu kwa wagonjwa.

Aidha, ameeleza kuwa Kairuki sasa ina Idara ya Huduma za Dharura yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 9,000 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kutoa huduma bora kwa changamoto za afya za dharura.




Na Mwandishi Wetu 

KAMISHNA wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema uzalishaji wa nishati nishati jadidifu ya maji na jua nchini umefikia asilimia 67.


Mhandisi Luoga ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya wataalam kutoka taasisi mbalimbali nchini yaliyohusu usanifu, utengenezaji na ufungaji wa mifumo ya Nishati ya Jua pamoja na matumizi yake.


"Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya bora ya nishati jadidifu ikiwa ni pamoja na Nishati Safi ya kupikia hasa baada ya nchi kutia saini Mpango Mahsusi wa Taifa wa Nishati mwezi Januari mwaka huu.


Moja ya miradi mikubwa tunayoitekeleza sasa katika nishati jadidifu ni mradi wa umeme jua wa  Kishapu mkoani Shinyanga ambao umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kuzalisha megawati 50 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajiwa kuzalisha megawati 100," amesema Luoga


Mhandisi Luoga amesema  mafunzo kuhusu teknolojia ya nishati ya jua yamefanyika nchini kwa sababu Tanzania imepiga hatua  kubwa katika matumizi bora ya nishati na nishati jadidifu.


Aidha,  amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya nishati jadidifu nchini.


Amesema washiriki kutoka katika taasisi mbalimbali wameshiriki mafunzo ya Nishati ya Jua yanayojulikana kama SOLTRAIN + ambayo yameandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kituo Mahiri cha Matumizi Bora ya Nishati na Nishati Jadidifu (SACREEE) ambacho kipo chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika ( SADC).


Awali, mafunzo hayo yalifunguliwa na Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambapo aliwataka washiriki hao kutumia ujuzi na maarifa waliyopata katika kujiajiri na pia kutoa ujuzi kwa wengine.


 

Juma Ramadhani, mjasiriamali kutoka Mkwajuni, alipongeza elimu aliyopata kuhusu Nishati Safi ya Kupikia na kuahidi kubadilisha mtindo wake wa maisha kwa kuanza kutumia nishati hiyo.

“Nimejifunza mambo mengi kuhusu faida za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Nitabadilika na nitakuwa balozi wa kuhamasisha wajasiriamali wenzangu na jamii kwa ujumla juu ya matumizi ya nishati hii,” alisema Ramadhani.



Wito wa kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umetolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kongamano la Wajasiriamali Wilaya ya Songwe, lililofanyika Agosti 16, 2025 katika kijiji cha Mkwajuni, mkoani Songwe. Kongamano hilo liliandaliwa na Mtandao wa Kuinua Wanawake Kiuchumi Tanzania (TAWEN) na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 350.



Mtaalam wa Nishati na Jinsia kutoka REA, Dkt. Joseph Sambali, alisema kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia.

“Wajasiriamali wanayo nafasi kubwa ya kufaidika na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani katika sekta ndogo ya Nishati Safi ya Kupikia,” alisema Dkt. Sambali.



Alitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na uwakala na uzalishaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia kama vile mkaa mbadala na majiko banifu. Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya ya mtumiaji na mazingira.

“Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ni muhimu katika kuepusha magonjwa yanayotokana na uvutaji wa hewa chafu inayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo salama. Pia husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa,” aliongeza Dkt. Sambali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWEN Nyanda za Juu Kusini, Oliva Hasukenye, alisema kuwa wao kama mtandao wanaunga mkono kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia na wamejipanga kuendelea kuhamasisha jamii kupitia majukwaa mbalimbali.

“Sisi TAWEN tunaunga mkono kampeni hii ya Nishati Safi ya Kupikia kwani maisha ya kutumia nishati isiyo safi na salama tumeyaishi, madhara yake tunayajua, na tumedhamiria kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kuelimisha jamii kuhusu madhara hayo,” alisema Hasukenye.

Aliongeza kuwa mjasiriamali anayepika kwa kutumia nishati safi hawezi kulinganishwa na yule anayetumia nishati isiyo salama, kuanzia kipato hadi usafi wa mazingira anayofanyia kazi.

Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kuelimisha, kuwezesha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, ili kulinda afya ya wananchi na kuhifadhi mazingira kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua kampeni mpya ya kitaifa inayolenga kuhamasisha wateja wake kulipa madeni na kulinda miundombinu ya umeme, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma endelevu ya umeme nchini.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TANESCO, Irene Gowelle, amesema kampeni hiyo yenye jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie” imezinduliwa rasmi leo tarehe 19 Juni 2025, ikibeba kaulimbiu isemayo “Huduma Endelevu Huanza na Wewe.”

“Malengo ya kampeni hii ni kuwahamasisha wateja wa malipo ya baada kulipa madeni yao kwa hiyari kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, na kutoa motisha kwa ulipaji wa wakati ikiwemo msamaha wa riba kwa wateja watakaolipa madeni yao kikamilifu,” amesema Gowelle.



 

Ameeleza kuwa kampeni hiyo pia itahusisha ukaguzi wa mita za LUKU kwa wateja wa malipo kabla, kwa lengo la kuhakikisha mita hizo zinafanya kazi ipasavyo na hazijafanyiwa udanganyifu na wateja wasio waaminifu.

“Tutahakikisha kuwa mita zote ziko katika hali nzuri na hazijachezewa. Zoezi hili ni muhimu kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya umeme na uadilifu katika mfumo wa usambazaji,” amesema.

Gowelle amesema kuwa TANESCO pia itaendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu ulinzi shirikishi wa miundombinu ya umeme, kwa kushirikiana na jamii na kuwajengea uelewa wa namna bora ya kulinda rasilimali za shirika hilo.

“Tunaendelea kuhimiza ulinzi wa miundombinu kwa kuwashirikisha wananchi. Tunataka jamii iwe sehemu ya suluhisho kwa kutoa taarifa na kulinda miundombinu inayowahudumia wao wenyewe,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wateja waliodaiwa na TANESCO kutoa ushirikiano kwa kulipa madeni yao kwa wakati ili kuzuia usumbufu wa huduma na kuepuka hatua za kisheria.

“Tunatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa umeme au uharibifu wa miundombinu kwa kushirikiana na vyombo vya dola. Hii itapunguza athari zinazoweza kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme na kuzuia hasara kwa shirika,” amesisitiza Gowelle.

Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za TANESCO kuhakikisha huduma ya umeme nchini inakuwa ya kuaminika, salama, na endelevu .

 


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) – Kanda ya Kaskazini, imewataka mawakala wa gesi za majumbani (LPG) kuhakikisha wanazingatia kanuni za usalama na sheria za upimaji wa uzito kabla ya kuwauzia wateja mitungi ya gesi, ikiwemo kutumia mizani na kuhakikisha mitungi ina “seal”. 


Wale watakaobainika kukiuka taratibu hizo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini au kunyimwa leseni za biashara.



Akizungumza Alhamisi, tarehe 19 Juni 2025, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wasambazaji na wauzaji wa LPG katika Jiji la Arusha, Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Longidu alisema:

“Tumewakumbusha hatua tutakazozichukua tukiwakuta mawakala wa gesi hawana mizani za kupimia uzito wa mitungi kabla ya kuwauzia wateja. Kama mitungi haina seal, tutawapiga faini.”

 

Aidha, Mhandisi Longidu alieleza kuwa EWURA inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.



“Mkakati huu unalenga kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao ni hatari kwa mazingira na afya,” alisema Longidu.

Meneja huyo pia alisisitiza wajibu wa watoa huduma kutoa elimu kwa wateja kuhusu usalama wa matumizi ya gesi:

“Wamesisitizwa kuelimisha wateja wao kabla ya kuwauzia mitungi ya gesi. Gesi isipotumika kwa usahihi inaweza kusababisha madhara makubwa.”


 

Mhandisi wa Petroli kutoka EWURA, Magreth Mwita, aliwaeleza washiriki utaratibu wa kupata leseni za kusambaza au kuuza LPG:

“Ni muhimu wafuate matakwa ya kisheria na ya kiufundi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji na uendelevu wa biashara.”

 


Kwa upande wa sekta binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa LPG Tanzania, Mhandisi Amos Mwansumbule, alisema:

“Tunawahimiza mawakala ni lazima watumie mizani ili mteja ahakikishe mtungi wake kabla hajauchukua. Lengo letu ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.”


 

Akitaja changamoto kubwa, Mwansumbule alisema:

“Sasa kumetokea watu wanajaza mitungi ya gesi kiholela mitaani. Wanachukua mitungi ya wanachama wetu na kuijaza kwa ujazo mdogo, mtu ananunua mtungi wa kilo sita kumbe ni kilo tatu. Tunataka kushirikiana na EWURA kuwadhibiti.”

Aliongeza kuwa wasambazaji wa gesi wana wajibu wa kutoa elimu ya matumizi salama kwa kila ngazi ya usambazaji:

“Katika mnyororo wa usambazaji wa gesi tuna wadau wanne: msambazaji mkuu, msambazaji wa kati (distributor), wakala wa mtaani, hadi mtumiaji wa mwisho. Kila mmoja anawajibika kutoa elimu kwa anayemfuata.”


 

Nganashe Laizer, ambaye ni wakala wa kuuza gesi jijini Arusha, alisema semina hiyo imemsaidia kuongeza uelewa:

“Leo nimejua kuwa kumbe tunatakiwa tuwe na mizani na ile mitungi inapaswa kuwekwa eneo la wazi lenye hewa ya kutosha, pamoja na kuonyesha bei elekezi.”

Hata hivyo, Laizer alilalamikia ushindani usio wa haki kutoka kwa wafanyabiashara wasiokidhi vigezo:

“Changamoto ni kwamba kuna watu wameingia kwenye biashara ya gesi bila vigezo. Mtu ana duka dogo tu, anaweka mitungi, wengine wanauza bei ya chini kuliko elekezi. Sisi tumewekeza fedha nyingi lakini tunaharibiwa.”

Alisema hali hiyo itapatiwa suluhu iwapo mamlaka zitasimamia utekelezaji wa sheria:

“Iwapo kila mmoja atazingatia sheria, vigezo, na kuweka mitungi sehemu salama na kwa bei elekezi, tutafanya biashara kwa haki.”

EWURA imeahidi kuendelea na kampeni za elimu kwa umma, ukaguzi wa mara kwa mara, na kuwachukulia hatua wafanyabiashara watakaoshindwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kulinda usalama wa wananchi na mazingira.

 




Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema ameridhishwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika Kituo cha Huduma za Pamoja cha Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya, na ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuharakisha ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme wilayani Longido ili kuboresha upatikanaji wa nishati katika eneo hilo.



Dkt. Biteko alitoa maelekezo hayo Aprili 24, 2025, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.



“Nimefurahishwa sana na namna mnavyohamasisha biashara. Mmekusanya shilingi bilioni 101 kati ya lengo la bilioni 124 huku zikiwa zimebaki miezi kadhaa kabla ya mwaka wa fedha kuisha. Hii ni hatua kubwa,” alisema Dkt. Biteko, akiipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kazi nzuri inayofanywa katika kituo hicho.



Aliwataka watendaji wa kituo hicho kuendelea kuboresha huduma kwa kupunguza muda wa kushughulikia mizigo kutoka saa mbili hadi dakika 30 hadi 40 ili kuharakisha biashara na kuongeza tija kwa wafanyabiashara.



Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko alitembelea pia Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia, ambapo alieleza kuwa Serikali kupitia Kampuni ya Taifa ya Gesi itasimamia ufungaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia shuleni hapo.



“Shule hii ni sehemu ya dira ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya nishati safi na salama. Tumejipanga kuhakikisha mfumo wa gesi unafungwa kwa gharama ya Serikali,” alieleza.



Aidha, alitoa maagizo kwa uongozi wa mkoa kuhakikisha shule hiyo inakamilisha maabara zote nne za sayansi kwa kuzipatia vifaa.



“Wanafunzi wasiendelee kuchora bunsen burner kwenye daftari. Waziione, wazitumie na wajifunze kwa vitendo,” alisisitiza Dkt. Biteko.



Pia alielekeza TANESCO kuhakikisha ndani ya wiki tatu nguzo 25 zinafikishwa kwenye vitongoji ambavyo bado havijaunganishwa na umeme. “Vijiji vyote 52 vina umeme lakini kati ya vitongoji 176, ni 112 tu vyenye umeme. Hali hii inapaswa kubadilika haraka,” alisema.



Dkt. Biteko pia alitoa maelekezo ya kujengwa kwa njia nne za kusambaza umeme kuelekea maeneo ya Loliondo, Namanga, Mundarara na Kamwanga, sambamba na ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Longido.



Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mundarara, Dkt. Biteko alieleza kuwa madini ni kichocheo kikubwa cha maendeleo, akitolea mfano wa uzalishaji wa madini ya rubi unaoendelea kijijini hapo.


“Nimefurahi kuona Watanzania sasa wana uwezo wa kushiriki katika shughuli za uchimbaji kwa ufanisi,” alisema.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Longido, Dkt. Steven Kiruswa, alisema wilaya hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.



“Wachimbaji wadogo wamepata umeme wa uhakika na katika kipindi cha miaka minne wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 9.9,”
alisema.



Dkt. Kiruswa aliongeza kuwa ujenzi wa shule mpya sita za sekondari unaendelea katika kata mbalimbali, huku kata tatu pekee zikiwa hazijafikiwa. Alieleza pia kuwa mgodi wa magadi soda wa Engaruka tayari umetengewa fedha na wawekezaji wapo tayari kuanza kazi.



Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI kuhusu ujenzi wa daraja, kituo cha afya na miundombinu mingine tayari yameanza kutekelezwa. 



“Zaidi ya shilingi milioni 250 zimetengwa kwa kituo cha afya na tayari zimeanza kuonekana kwenye mfumo wa fedha. Barabara ya Resingita imetengewa milioni 270, na barabara ya Longido kwenda Meloe imetengewa milioni 105,” alisema.



Dkt. Biteko alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo. 



Alisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kutathmini mchango wake katika jamii na kwa taifa.