Mtuhumiwa wa Utekaji Mtoto Akamatwa na Kupigwa Risasi Akijaribu Kutoroka

 



Polisi: "Hatutasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria"

Dar es Salaam, Machi 9, 2025 – Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemkamata na baadaye kumjeruhi kwa risasi mtuhumiwa wa utekaji mtoto, Stanley Dismas Ulaya (18), mkazi wa Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumteka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8, mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mbezi, Ubungo, jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilitokea Machi 6, 2025, wakati mtoto huyo aliposhuka kwenye daladala kuelekea shuleni, ndipo mtuhumiwa alimkamata na kumpeleka hadi Bagamoyo, mkoani Pwani, ambako alimficha vichakani huku akitumia namba ya simu ya mzazi iliyokuwa kwenye madaftari ya shule ya mtoto huyo kudai pesa kwa vitisho.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, alisema kuwa Jeshi la Polisi lilifanya juhudi kubwa za ufuatiliaji hadi kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa mnamo Machi 8, 2025, majira ya saa 1:00 usiku.

"Baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, mtuhumiwa alijaribu kutoroka kwa kukimbia. Askari walilazimika kupiga risasi hewani kwa tahadhari, lakini alipokaidi, walimlenga kwa risasi mguuni na pajani ili kumzuia," alisema Kamanda huyo.

Mtuhumiwa alipelekwa hospitalini kwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata, huku hali ya mtoto ikiendelea kuwa nzuri chini ya uchunguzi wa madaktari.

Jeshi la Polisi limeendelea kulaani vikali vitendo vya utekaji nyara na limeahidi kuchukua hatua kali kwa wahusika wote kwa mujibu wa sheria. "Hatutasita kuwashughulikia wahusika wa vitendo hivi kwa mujibu wa sheria. Tunatoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu," aliongeza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


0 Comments:

Post a Comment