Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amewataka wananchi kulinda mawasiliano yao ya simu kwa umakini kama wanavyolinda mali zao zenye thamani.
Katika kikao hicho kilichofanyika pembeni ya uzinduzi wa kampeni ya Sitapeliki, Waziri Silaa alieleza kuwa ulinzi wa simu unapaswa kuwa kipaumbele cha kila mtu ili kuepuka kutapeliwa.
"Usijiunge na link usizozifahamu, ukijiunga nayo kwa mfano kwenye Facebook, imetengenezwa kwa mfumo unaoiwezesha kuchukua akaunti yako.
Wakishachukua akaunti yako wanaitumia kuomba watu fedha kwa kuandika vibonzo vya kulaghai watu," alisema Waziri Silaa.
Aliongeza kuwa, "Kuclick link usiyoifahamu ni kama kugongewa mlango nyumbani kwako usiku na mtu usiyemfahamu kisha umfungulie. Yaani mtu anagonga unamuuliza nani hakujibu au anakwambia mimi mbunge wako au nakwambia mimi mwanamaombi halafu umfungulie unakuta umemfungulia mwizi ndiyo hivyo hivyo utakavyoclick link usiyoijua unakua umefungulia wezi."
Waziri Silaa alisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kutoa taarifa kwa polisi pindi wanapojitokeza matukio ya utapeli kupitia mitandao ya simu.
Alihimiza wananchi kuwa na tahadhari na kutoa taarifa haraka wanapopoteza simu au kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa mawasiliano yao.
"Watanzania wakipoteza line waone ni jukumu lao kutoa taarifa kwa mtoa huduma ili line ifungwe.
Mtu ana simu ndogo ya 20,000 anapoipoteza haoni sababu ya kutoa taarifa kwa mtoa huduma na ni rahisi simu hiyo kuokotwa, na simu hiyo haina namba ya siri au una namba ya siri rahisi unakuta 1234," aliongeza.
Akiendelea kutoa wito wa kuchukua tahadhari, Waziri Silaa alisema kuwa mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha uhusiano kati ya matapeli na makampuni ya simu.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuna ushirikiano wa aina fulani unapotokea wakati matapeli wanapopiga simu kwa kutumia namba za simu za wahanga.
Kuhusu kampeni ya Sitapeliki, Waziri Silaa alitoa wito kwa kila mtanzania kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya utapeli kwa kutokutoa ushirikiano kwa matapeli.
Alisisitiza umuhimu wa kuweka namba za siri na kuepuka kufungua links ambazo hazijulikani.
"Kampeni ya Sitapeliki ni ya kila mmoja wetu kuweza kuamua kwamba hatapeliki, kwa kutokutoa ushirikiano, kuweka namba za siri, ambazo zina ugumu wa aina fulani wa mtu kuweza kubaini," alisema.
Pia, alitoa wito kwa watanzania kutambua kuwa hakuna pesa za bure zinazoweza kutolewa kupitia mitandao ya simu, hivyo wanapaswa kuwa makini na jumbe za utapeli ambazo hutumwa kwa njia ya links.
Baadhi ya waandishi wa habari walitoa maoni yao kuhusu huduma za simu na mitandao.
Walishauri kampuni za simu kutoa huduma za haraka kwa watumiaji ili kurahisisha utoaji wa taarifa na kuimarisha huduma nzuri kwa wananchi.
Kampeni ya Sitapeliki imezinduliwa kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu hatari ya utapeli kupitia mitandao ya simu na kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na uelewa zaidi kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya matapeli.




0 Comments:
Post a Comment