Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema chama hicho kinataka viongozi kuwaheshimu wananchi ambao ndio wapigakura wao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Lamadi, mkoani Simiyu, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu achaguliwe kushika nafasi hiyo, Heche alisema baadhi ya viongozi hawaheshimu kura za wananchi, hali inayowafanya kushindwa kuwahudumia ipasavyo.
"Tunataka viongozi waheshimu kura za wananchi, tunataka rasilimali za nchi hii zitumike kuwanufaisha wananchi," alisema Heche.
Aidha, alieleza kuwa vijana wengi wanagundua maeneo yenye madini, lakini wanapojaribu kuyatumia, hujikuta wakizuiwa na watu wenye leseni waliokuja kutoka mijini, hali inayosababisha vijana hao kubaki bila faida yoyote.
"Kuna vijana wanagundua machimbo, lakini kesho yake wanakuja watu kutoka mjini wakiwa na leseni tayari, vijana wanaambulia kupigwa na polisi," aliongeza.
Heche alisema maisha ya ukwasi kwa baadhi ya viongozi yamewafanya kushindwa kutambua changamoto wanazopitia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
0 Comments:
Post a Comment