Gambo Adaiwa Kutimka Kikaoni, Diwani Amwaga Machozi Akimsihi Makonda Agombee Ubunge Arusha Mjini




MADIWANI jiji la Arusha  wamshutumu Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo (CCM), wakidai kuwa amekuwa kikwazo kwa maendeleo ya jiji hilo hivyo kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kugombea ubunge wa Arusha Mjini kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.



Wameyasema hayo Kikao maalum cha bajeti cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha kilichofanyika Februari 24, 2025 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jiji hilo



Katika hali ya kushangaza, Gambo aliripotiwa kuondoka ghafla baada ya kupata taarifa kuwa Makonda anakuja kuhutubia kikao hicho, jambo lililoibua mjadala mkubwa miongoni mwa madiwani.


Diwani wa Kata ya Themi, Lobora Petro (CCM), alieleza kwa hisia kali namna ambavyo Gambo alipata taarifa za ujio wa Makonda na kuondoka haraka kabla ya Mkuu huyo wa Mkoa kufika.


"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, (Gambo) alikuwa umekaa hapa. Huyu jamaa aliposikia unakuja alipita hapa utafikiri amechomwa moto! Maana yake uongo na ukweli vinajitenga," alisema Lobora huku akishangiliwa na baadhi ya madiwani wenzake.


Lobora aliongeza kuwa Gambo amekuwa akiwakwamisha madiwani na maendeleo ya Jiji la Arusha.


"Tunakuhitaji kwa sababu tunataka mtu atakayeonyesha njia. Baraza hili limekwama kwa sababu ya mbunge. Mimi ninalia rohoni kwa sababu ninajuta kumuunga mkono kichwa cha mwendawazimu!" alisema huku machozi yakimtoka.


Aliendelea kusema:


"Tulikosea, tulimchagua mtu asiyejitambua! Narudia tena kukuomba msamaha kwa niaba ya wananchi wa Arusha. Tunakuhitaji na Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) aone tunakuhitaji Arusha mara mbili. Wewe si mtoto wa Arusha? Wewe si umeoa Arusha?"


Madiwani Wataka Makonda Agombee Ubunge



Diwani wa Kata ya Kimandolu, Ibrahim Mollel, naye alimuunga mkono Makonda kwa kusema:


"Watu wakisema, na sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Muda ukifika, chukua fomu, tuko nyuma yako! Leo umekaa hapa, Mungu akinirudisha, naomba nikae pale na wewe ukae hapa kama mbunge. Chukua hayo maneno, endelea kuyatafakari."


Madiwani waliendelea kusisitiza kuwa wanahitaji mbunge anayefanya kazi kwa vitendo na kushirikiana na viongozi wengine badala ya kuwakwamisha.


Kilio cha Wafanyakazi wa General Tire

Diwani Lobora pia alimueleza Makonda kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa General Tire waliodai kunyimwa haki zao.


"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kuna wafanyakazi wa General Tire wamenyimwa haki zao za msingi. Walitengeneza kabrasha kwa gharama ya shilingi 50,000 na nikampa mtu ambaye nilidhani angefanyia kazi, kumbe alilitupa. Badala yake akamleta waziri na kumshauri eneo hilo ligawanywe kuwa viwanja vidogo vidogo!" alisema diwani Lobora kwa uchungu.


Alisema hata alipolifikisha suala hilo kwa viongozi wa juu, alifanikiwa kusababisha waziri huyo kuondolewa, lakini bado wafanyakazi hawajapata haki zao.


"General Tire ina wafanyakazi zaidi ya 3,000 wanaodai haki zao. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, ukiniruhusu nitakuletea kabrasha lao na wawakilishi wao ili waone Mungu wa Makonda yupo Arusha na atawatetea na watapata haki zao," alisema diwani huyo.


Makonda Ataka Miradi Kukamilishwa



Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliwataka madiwani kuhakikisha miradi yote ya viporo inakamilika kwa wakati.


"Haiwezekani miradi inapoanza maneno yanakuwa mengi ilhali wananchi wanahitaji maendeleo. Hakikisheni miradi yote viporo inakamilika kwa wakati lakini pia pandeni miti, msipande fitna," alisema Makonda.


Aliendelea kusisitiza kuwa anataka Arusha kuwa mkoa wa mfano na kwamba hatakubali kupungua kwa mapato waliyojiwekea.


"Nataka Mkoa wa Arusha kuwa namba moja kwa kila kitu. Hatuwezi kukubali kupunguza mapato, tunataka kuongeza mapato ili maendeleo yaweze kufanyika katika kila kata," alisema Makonda.


Madiwani Wampongeza Makonda

Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Ibrahim Mollel, alimpongeza Makonda kwa kazi kubwa anayofanya katika mkoa huo na kusisitiza kuwa wananchi wanamuunga mkono.


"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kuna maneno ya kwenye Biblia yanayosema mfalme yeyote ni yule anayetoka kwenye jamii ndogo na anaandaliwa. 


Sisi tunasikia tunakaa na watu na wanasema juu yako kwa namna unavyogusa maisha ya wananchi," alisema Mollel huku madiwani wakipiga makofi.


Aliongeza kuwa Makonda ni mtu wa vitendo na anastahili kupewa nafasi kubwa zaidi ya uongozi.


"Sisi ni wale watu ambao tumepangiwa watu kuja kugombea kwenye kata zetu lakini mimi siogopi. Nimeshakuwa mwenezi wa wilaya, ni Mungu kaniweka. Nimekuwa diwani, ni Mungu kaniweka. Na leo umekaa hapa, Mungu akinirudisha, naomba nikae pale na wewe (Makonda) ukae hapa kama mbunge," alisema.


Juhudi za kumpata Gambo kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kuita muda wote bila kupokelewa.

0 Comments:

Post a Comment